Meza
Kuu ikiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu
Kijaji (Mb), (watatu kushoto) wakiimba
wimbo wa kudumisha umoja kabla ya kuanza Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo,
Jijini Dodoma. (Picha
na Kitengo cha Mawasilino Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango).
Mwenyekiti wa Baraza la
Wafanyakazi na Katibu Mkuu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Bw.Doto James akitoa
salam za utangulizi kwa mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Ashatu Kijaji (hayupo pichani), wakati
wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo lililofanyika katika ukumbi
wa Kambarage, Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb), akizungumza wakati
wa kufungua Baraza la Wafanyakazi, Jijini Dodoma, ambapo aliagiza Watendaji wa
Wizara hiyo kuendelea kuboresha mifumo ya kukusanya mapato ya ndani ikiwa ni
pamoja na kupanua wigo wa walipa kodi.
Meza
Kuu (waliyokaa) ikiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb),(watatu kushoto),
wakiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara hiyo
wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo lililofanyika katika
ukumbi wa Kambarage, Jijini Dodoma.
Na Farida Ramadhani & Josephine Majura. WFM, Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji , amewataka
Watumishi wa Wizara hiyo kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato
ya ndani na kupanua wigo wa walipakodi pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa
mapato kutoka vyanzo mbalimbali.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo
Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo
uliofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, wizarani hapo.
Alisema Wizara ya Fedha na
Mipango imebeba majukumu ya
kuhakikisha kuwa mapato ya Serikali na matumizi ya rasilimali fedha
yanasimamiwa kikamilifu.
“Watendaji na watumishi wote wa Wizara wanawajibu
wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha na ufuatiliaji wa matumizi ili
kuhakikisha rasilimali fedha zilizopo zinatumika kwa ufanisi” ,alisema Dkt. Kijaji.
Alisema
ni jukumu la Watumishi wa Wizara kugawa rasilimali fedha kwa
kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo
wa Miaka Mitano (2016-2021) wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili
kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.
Aliwataka Watumishi kufanyakazi kwa ushirikiano, umoja ,
mshikamano, ufanisi na uadilifu kwa
kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali iliyopo.
“Ni wajibu wetu pia
kutumia busara na hekima, hususan pale tunaposhughulikia maslahi ya watumishi
na wananchi kwa ujumla”, alisisitiza Dkt. Kijaji.
Kwa upande wake Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Bw. Doto
James, amemhakikishia Dkt. Kijaji kuwa watatekeleza maelekezo yote aliyoyatoa
kwa haraka na ukamilifu kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa Wizara hiyo ni nguzo ya
kusimamia uchumi wa nchi.
Alisema uzoefu unaonesha
kwamba vikao vya Baraza la wafanyakazi vimekua na umuhimu mkubwa mahala pa kazi
na kwa kuzingatia umuhimu huo Wizara ya Fedha na Mipango imehakikisha kuwa vikao
vya Baraza vinafanyika kila mwaka kulingana na Mkataba kati ya Wizara na Chama
cha Wafanyakazi cha Serikali na Afya (TUGHE).
Alisema
kupitia Baraza la wafanyakazi Wizara imefanikiwa kuongeza mshikamano kati ya
Wafanyakazi hivyo kuamsha ari kwa watumishi kufanya kazi kwa kushirikiana na
Viongozi wa Serikali.
Aliongeza
kuwa hoja mbalimbali zilizowasilishwa kwenye Baraza zimeboresha huduma kwa
watumishi, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ikiwemo kuwapatia watumishi
vitendea kazi pamoja na kuwelimisha watumishi kuhusu magonjwa sugu kama vile
kisukari, shinikizo la damu (BP), Kifua kikuu, HIV na UKIMWI.
No comments:
Post a Comment