HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 11, 2019

WAZIRI MKUU: SERIKALI ITAWEZESHA VIONGOZI WAPATE MAFUNZO YA UONGOZI NA MAADILI

Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, wakati alipo wasili kufungua kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere Aprili 11, 2019, katika Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen Wasira, wakati alipo wasili kwenye ufunguzi wa kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere Aprili 11, 2019, Kigamboni jijini Dar es Salaam. Tokea kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Shadrack Mwakalila, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, kwenye ufunguzi wa kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere Aprili 11, 2019, katika Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam. Katikati ni Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa akitoka kwenye jengo la Utawala la Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam, kabla ya kufungua kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere Aprili 11, 2019. Kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen Wasira, kwenye ufunguzi wa kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere yaliyofanyika katika Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam Aprili 11, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen Wasira, akitoa hotuba yake.
 Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako,akitoa hotuba yake.
 Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia, kwenye ufunguzi wa kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam Aprili 11, 2019.
 Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia, kwenye ufunguzi wa kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam Aprili 11, 2019.




WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaangalia uwezekano ili viongozi wa ngazi mbalimbali wapate mafunzo ya uongozi na maadili kwenye Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kama sehemu ya kurejesha maadili kwa viongozi.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 11, 2019) wakati akifungua kongamano la Kumbukizi ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililofanyika kwenye chuo hicho, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Amesema Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Manispaa, Miji na Wakuu wa taasisi mbalimbali za umma wanastahili kupelekwa kwenye chuo hicho ili wapigwe msasa juu ya maadili ya uongozi.

“Kwa viongozi wetu wote kuanzia Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurgenzi wa Halmashauri na Wakuu wa taasisi mbalimbali za umma ambao wanatakiwa kujengewa msingi imara wa namna ya kuongoza, hapa ndiyo mahali pake. Nalichukua ombi lenu ili tuwape fursa ya wiki moja au mbili waje hapa wajifunze miiko ya uongozi,” amesema.

“Wanatakiwa waje kupata namna ya kuwa kiongozi, miiko ya namna kiongozi anavyotakiwa awe. Unapokuwa kiongozi unatakiwa ujue mambo gani unapaswa uyaache. Unapokuwa kiongozi kuna baadhi ya mambo unatakiwa uyaache. Hata kama ulikuwa umezoea kushangilia mpira kwa kuvua shati, ukiwa kiongozi unaacha kuvua shati.”

Amesema kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia hakuna namna ya kukwepa kujifunza na kupata maarifa mapya huku akinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwl. Julius K. Nyerere ambaye aliwahi kusema: “…Watu walio hatari sana ni wale ambao wanafikiri kuwa wanajua kila kitu, wala hawana haja kujifunza zaidi. Hii ni tabia mbaya ambayo huzuia kabisa maendeleo.”

“Napenda kuwahakikishia kuwa nimepokea changamoto hii ya msingi na tutazama namna nzuri ya kuwezesha viongozi katika ngazi mbalimbali waje kupata mafunzo ya uongozi katika chuo hiki.”

Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Shadrack Mwakalila kwamba mwitikio wa viongozi na watendaji wakuu wa Serikali kushiriki katika mafunzo ya uongozi, maadili na utawala bora umekuwa hafifu licha ya jitihada kubwa za kutangaza mafunzo haya kupitia njia mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ombi lililotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Mzee Stephen Wassira la kutaka chuo hicho kipandishwe hadhi na kuwa chuo kikuu ni jambo linalowezekana kwa sababu waziri mwenye dhamana ya elimu ya juu nchini alikuwepo na amesikia ombi lao.

“Mwelekeo wa chuo ndiyo unaotiliwa mkazo na Serikali hii, jina lenyewe la chuo ni tunu. Kama Tanzania tuna chuo chenye jina la Waziri Mkuu, tutashindwaje kutoa jina kwa muasisi wa nchi yetu? Mheshimiwa Waziri uko hapa, libebe suala hilo na ulifuatilie.”

Mapema, Mzee Wassira alitoa maombi matatu la kwanza likiwa ni kutaka chuo hicho kipewe hadhi ya kuwa chuo kikuu na jina lake libadilishwe na kuwa Mwalimu Nyerere Memorial Leadership University. Pia aliomba mazingira ya chuo yabadilishwe ili yalingane na hadhi ya mwenye jina.

Pia Mzee Wassira aliomba Serikali ikitumie chuo hicho kuendeleza kazi iliyokuwa ikifanywa na chuo cha Kivukoni ya kuwaandaa viongozi kwa kuwapa mafunzo juu ya maadili ya uongozi na kuongeza kuwa wakipata mafunzo ya wiki moja au mbili ni lazima watabadili mitazamo yao.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na balozi wa Namibia hapa nchini Bibi Theresia Samaria, balozi wa Msumbiji hapa nchini Bibi Monica Patricio Clemente, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye alikuwa mwenyekiti wa kongamano hilo. Wengine ni mawaziri wastaafu wa Serikali ya awamu ya kwanza, Mzee Ibrahim Kaduma, na Mama Thabitha Siwale. Wengine ni Mzee Wilson Mukama na Bw. John Shibuda.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
 S. L. P. 980,
 41193 – DODOMA,                      
ALHAMISI, APRILI 11, 2019.

No comments:

Post a Comment

Pages