HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 15, 2019

Woods bado moto chini, abeba taji la Masters

BAADA ya ukame wa miaka 11 ya mataji, nyota bora wa dunia katika mchezo wa gofu, Tiger Woods (pichani) amerejea katika ubora wake baada ya kutwaa taji la michuano ya Masters, ikiwa ni ishara kuwa mkali huyo ameanza kurejesha makali yake.

Kati ya vitu vilivyomfanya nyota huyo akapoteza makali yake dimbani, ni pamoja na kashfa ya ngono, hali ya kuwa majeruhi hadi kufanyiwa upasuaji na msongo wa mawazo, lakini sasa Woods, amerejea katika ubora wake akiruka vihunzi vyote vilivyokuwa vimeyasonga kipaji chake.

Ingawa ulikuwa ni mchuano wa nyota sita katika hatua ya fainali, lakini watano kati yao walifungana, wakimwacha Woods kuweka rekodi ya kuanza hatua za kurejesha makali yake kama vile ndo kwanza anatwaa taji la kwanza mwaka 1997.

Tofauti ni kwamba, wakati mwaka huo Woods alitwaa taji lake la kwanza la kimataifa, juzi alibeba taji hilo la 15 katika historia yake, likipatikana baada ya ukame wa miaka 11 ya kushindwa kufanya hayo kutokana na sababu kadha wa kadha.

Baada ya Woods akiwa katika mavazi ya rangi ya njano kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ya kimatifa, uwanja ulizizima kwa shangwe na mayowe kwa kuita; Tiger! Tiger! Tiger!”.

Kwa mafanikio hayo, uso wa Woods ulionekana ukiwa katika tabasamu murua kabla ya kukumbatiwa na mwanaye wa kiume aitwaye Charlie ambaye wakati mkali huyo anatwaa taji la kwanza miaka 22 iliyopita, hakuwa amezaliwa.
 “...Wakati napiga kuingiza katika shimo, sikueleza ni kitu gani ninafanya, ajapo nilijua kuwa ninachokifanya kinaonekana kupitia runinga.

“Kuyafanya haya mbele ya mwanangu, ni furaha isiyo na kifani. Wakati natwaa taji langu la kwanza mwaka 1997, baba yangu alikuwepo, nami sasa ni baba,” alisema Woods mbele ya mwanaye mwenye umri wa miaka 10.

Woods, pia ametambua ubora wa wapinzani wake kama Brooks Koepka, Francesco Molinari na wengine ambao wamekuwa wakishiriki michuano hiyo kwa mafanikio makubwa

No comments:

Post a Comment

Pages