*Amwagiza Katibu Mkuu Kilimo atume timu ichunguze Bodi ya Pamba
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa dharura wa baadhi ya wadau wa zao la pamba wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa wakati alipozungumza katika mkutano aliouitisha kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa dharura wa baadhi ya wadau wa zao la pamba wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa wakati alipozungumza katika mkutano aliouitisha kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema ana imani kuwa ununuzi wa zao la pamba
utaanza mara moja kwa bei ya sh. 1,200 kwa kilo moja katika mikoa yote
inayozalisha zao hilo.
Amefikia
uamuzi huo baada ya kuwepo kwa sintofahamu ya bei kwa takriban ya wiki
nne tangu bei elekezi ilipotangazwa Aprili 30, 2019 mkoani Shinyanga
kwamba bei hiyo ianze kutumika kuanzia Mei 2, 2019.
Alikuwa
akizungumza na wadau wa sekta ndogo ya pamba kwenye kikao
kilichofanyika leo (Jumatano, Mei 29, 2019) kwenye ukumbi wa Chuo cha
Benki Kuu, jijini Mwanza. Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Mawaziri wa
Kilimo na Viwanda, Makatibu Wakuu wa Kilimo na Ofisi ya Rais – TAMISEMI
na Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu na Geita.
Wengine
ni wawakilishi wa Wabunge wa mikoa hiyo, Makatibu Tawala wa mikoa,
Wakuu wa Wilaya zote za mikoa hiyo, na Wakurugenzi wa Halmashauri za
Wilaya hizo. Pia kilihudhuriwa na wanunuzi wa pamba, wakulima na maafisa
wa benki kadhaa.
Waziri
Mkuu aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba Serikali bado inaendelea
kutafuta njia nzuri ya kuwakutanisha wadau wa mazao ya kibiashara ili
yaweze kuwa na tija kwa wakulima. Alisema kazi hiyo inafanywa wa Wizara
ya Kilimo. Mazao hayo ni pamba, chai, kahawa, korosho, tumbaku na
chikichi.
Pia
alisema Bodi ya Pamba iachiwe jukumu la kutoa leseni za ununuzi wa zao
hilo na kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri waliokuwa wakifanya kazi hiyo
waache mara moja. “Kuna baadhi ya Wakurugenzi wanatoa leseni za ununuzi,
lakini wenye Mamlaka ni Bodi ya Pamba. Mnunuzi nenda Bodi ukapate
leseni yako,” alisema Waziri Mkuu.
Alitumia
fursa hiyo kuwakemea baadhi ya wakurugenzi ambao wamekuwa wakizuia
wanunuzi wapya kwenye maeneo na kuendelea kuwakumbatia wanaowataka wao.
“Wakurugenzi baadhi yenu mnazuia wanunuzi wapya, mnamtaka fulani tu. Kwa
kufanya hivyo, unapungua kiwango cha kilo ambacho wakulima wako
wangeuza,” alionya.
‘Wanunuzi
nendeni mkajitambulishe kwa Wakuu wa Wilaya au Wakurugenzi ili watambue
kwamba mpo kwenye maeneo yao lakini kila mnunuzi anayo haki ya kwenda
kununua pamba mahali popote hapa nchini.”
Kuhusu
ubora wa pamba, Waziri Mkuu alitaka wananchi waelimishwe ili waache
kuweka maji au mchanga kwenye pamba kwa minajili ya kuongeza uzito kwani
kwa kufanya hivyo wanachafua jina la Tanzania pindi inapopelekwa kuuzwa
nje ya nchi.
Pia
alitaka vyama vikuu vya ushirika vijiridhishe kuhusu ubora wa maghala
ya kuhifadhia pamba kwenye vyama vya msingi (AMCOS) kwani kwa kufanya
hivyo, itawasaidia wakulima wauze mapema pamba yao mara baada ya
kuivuna.
Kuhusu
mizani, Waziri Mkuu aliiagiza wakala wa vipimo nchini (WMA) waende
wakakague mizani ya kwenye AMCOS na kwenye vinu vya kuchambulia pamba
(ginneries) kwa sbabu ya tofauti kubwa ya uzito inayojitokeza na
kuwalazimisha wakulima kulipia upotevu wa kilo hizo.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew
Mtigumwe atume wakaguzi kwenye Bodi ya Pamba ili wabainishe matumizi ya
sh.100 kwa kila kilo ambazo zimekuwa zikilipwa kwenye bodi hiyo.
“Katibu
Mkuu Kilimo lete wakaguzi ndani ya bodi ya pamba, waangalie kwa kipindi
cha miaka mitatu toka tulipoanza kukusanya sh. 100 kwa kilo,
zimekusanywa shilingi ngapi, na zimetumika kulipia nini.
“Na
Mrajisi wa Ushirika nchini ufanye ukaguzi kwenye vyama vikuu vya
Ushirika na AMCOS. Uangalie ziko ngapi na zinafanya nini. Kuna AMCOS
zina hela, je fedha hiyo imetumika kufanya nini ili kuendeleza zao la
pamba. Je zimenunua matrekta au zimelipia posho za vikao,” alisema.
Naye Mwenyekiti
wa Chama cha Wanunuzi Binafsi wa Pamba (TCA), Bw. Christopher Gachuma
ameshukuru Waziri Mkuu kwa maelekezo aliyoyatoa kuhusu utoaji wa leseni
kwani yalikuwa ni kikwazo kikubwa kwa baadhi ya wanunuzi wa zao hilo.
“Suala
la utoaji leseni linapaswa lianze mapema lakini kuna wengine hadi sasa
bado hawajapata leseni zao.” Aliwataka wanunuzi wa pamba waanze kununua
pamba ili msimu wa mauzo uanze kwa kasi.
No comments:
Post a Comment