Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, amesema kuwa ukweli kuhusu kifo cha Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, anaujua mtoto wake Regina na mdogo wake Benjamin Mengi, ambao wako Dubai.
Kikwete ambaye alikuwa miongoni mwa Viongozi
waliofika nyumbani kwa marehemu Dk. Mengi kutoa pole, alisema watu
waache uongo na kuongea mambo yasiyokuwepo kuhusiana kifo cha bilionea huyo.
Tangu kilipotokea kifo cha Dk. Mengi, kumekuwa na maneno na
taarifa nyingi mtandaoni, zikieleza taarifa tofauti ambazo nyingi zinadaiwa
kuwa ni za uongo na uchonganishi.
Kikwete ametoa kauli hiyo
jana wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya
kusaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Dk. Mengi Kinondoni, jijini Dar es
Salaam.
Alisema kama kweli watu
walikuwa wanampenda Dk. Mengi, basi mambo ya uongo na ya kutunga wanapaswa
kuyaacha na kusubiria watu waliopo Dubai wanaoshughulikia kurejesha mwili wa
marehemu, kutoa taarifa sahihi juu ya kifo hicho ambacho kimetikisa nchi.
"Tunajua Dk. Mengi amefariki
dunia akiwa Dubai ila Benjamini ambaye ni mdogo wa marehemu yupo huko na binti
yao Regina Mengi, yupo pia kwa hiyo hao ndio wenye ukweli hivyo wakirudi
watatuambia nini hasa kilitokea na ilikuaje, ombi langu ni hilo na haya maneno
yangu sasa msije mkayachanganya, " alisema.
Kikwete alisema kuendelea kwa
maneno hayo ya uongo kutasababisha kuichanganya jamii hivyo watu wanapaswa
kuacha kuyasema mambo hayo na kuwa wavumilivu mpaka wale waliopo Dubai
watakaporudi nchini na kutoa taarifa sahihi.
Hata hivyo alisema kuwa kifo
cha Dk. Mengi kimestua wengi na ni pigo kubwa kwa Taifa lakini hawezi
kuacha kuukubali ukweli kwamba kila nafsi itaonja umauti.
Alisema Taifa limepoteza
raia makini, mchapakazi na mzalendo hivyo watamkumbuka Dk. Mengi
kwani amechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi hii kwa kuwasaidia watu
mbalimbali wakiwemo maskini na walemavu.
"Najua tulitamani sana
kama Taifa kuwa naye lakini ndo hivyo Mwenyezi Mungu amempenda zaidi na
ameshapitisha uamuzi wake hata hivyo tuelewe kuwa kwa sababu yoyote na
kwa mazingira yoyote ile kila mtu ataondoka hapa duniani, nawatakia moyo
wa subra ndugu jamaa na marafiki," alisema Mzee Kikwete.
Alisema kabla ya umauti kumkuta,
alizungumza na kusalimiana naye kwa sababu alikuwa kama kaka yake na kuongeza
kuwa walikubaliana naye kwamba akirudi safari nchini Benin, watakutana na
kuzungumza.
Alisema Dk. Mengi amefanya
mengi na hivyo ni muhimu yale aliyoyafanya hapa duniani yadumushwe na yaendelee
kufanyika na kuongeza kuwa watu waendelee kuwa watulivu katika kipindi hiki.
Aidha alisema watamkumbuka
marehemu Mengi kwani alikuwa mtu mwenye huruma na moyo wa kusaidia watu
mbalimbali na ametumia utajiri wake kuwasaidia Watanzania wengi.
IGP Sirro.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini (IGP) Simon Sirro alisema kuwa wameona kinachoendelea katika mitandao ya
kijamii na tayari wameshafungua dokezo na wameshaanza kufuatilia
taarifa zinazotolewa na watu mbalimbali katika mitandao hiyo kuhusu kifo cha
Dk. Mengi.
"Tumeona na tunafuatilia
taarifa mbalimbali zinazotolewa katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Mzee
Mengi hatuzipuuzii ila kwa sasa kazi ni kuhakikisha msiba unamalizika kwa
amani na utulivu, "alisema Sirro.
Alisema Jeshi la Polisi
limejipanga kuimarisha ulinzi siku ya kutoa heshima za mwisho ambayo anaamini
kutakuwa na waombelezaji wengi ili watu wenye nia ovu wasipate nafasi ya
kuharibu zoezi hilo.
Alisema kifo cha Dk. Mengi ni
pigo kubwa kwa Jeshi hilo kwani alikuwa mdau muhimu na alilipenda Jeshi
tofauti na wafanyabiashara wengine.
"Mengi ni mtu aliyekuwa na
fedha lakini alikuwa tofauti na matajiri wengine hakika Jeshi letu limepoteza
mdau mkubwa sana kwa sababu alilipenda Jeshi na alikuwa mzalendo na tofauti na
wafanyabiashara wengine ambao wanaliona Jeshi adui kutokana na mambo
wanayoyafanya ikiwemo kuvunja Sheria," alisema Sirro. Chanzo Gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment