Serikali inatekeleza mpango
mkakati wa kujenga Kituo kikumbwa cha Biashara cha Afrika Mashariki katika eneo
la Nyakanazi Mkoani Kagera ili kuwanufaisha wananchi wanozunguka eneo hilo na
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki- EAC.
Hayo yameelezwa Bungeni
jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (pichani), alipokuwa
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalaum Mhe. Halima Abdalallah
Bulembo, alieuliza kuhusu mpango wa Serikali wa kujenga Kituo cha Biashara
katika mkoa wa Kagera unaopakana na nchi nyingi za EAC.
Dkt. Kijaji alisema kuwa,
ujenzi wa Kituo cha Biashara eneo la Nyakanazi utawezesha wananchi wa Tanzania
pamoja na nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda
kulifikia soko hilo.
Akijibu swali la Msingi la
Mbunge huyo kuhusu mpango wa Serikali wa kuifanya Kagera ifaidike na uchumi wa
kijiografia, Dkt. Kijaji alisema kuwa, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali
ya kimkakati mkoani humo ukiwemo mradi wa Reli yenye kiwango cha Kimataifa
(SGR) kipande cha Isaka- Rusumo chenye urefu wa kilometa 371 na ukarabati wa
barabara ya Lusanga- Rusumo yenye urefu wa kilometa 91.
Aidha inatekeleza mradi wa
umeme wa megawati 80 katika mipaka ya Rusumo na Mtukula kwa ajili ya kuimarisha
shughuli za kibiashara na nchi jirani za Rwanda na Uganda.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji
alisema, mazao ya wakulima wa Kagera na bidhaa za baadhi ya viwanda vya
kusindika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu vinafaidika kimasoko na
jiografia ya Mkoa huo ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kusindika minofu ya Samaki
cha Fish Co Ltd na Supreme Perch Ltd.
Viwanda vingine ni Ambiance
Distillers Tanzania Ltd kinachozalisha vinywaji vikali, Bunena Development Co. Ltd,
NK Botling Co. Ltd na Kabanga Bottlers Co. Ltd vinavyozalisha maji ya kunywa na
kiwanda cha Mayawa kinachosindika wine ya
Rosella na juisi.
Alisema kuwa, sambamba na
utekelezaji wa miradi ya kimkakati, Serikali kupitia Mamlaka ya Biashara (Tan
Trade), ilitoa mafunzo ya kuhamasisha kuanzishwa kwa vikundi vya kurasimisha
biashara mipakani katika vituo vya Kabanga, Rusumo na Mtukula vinavyopakana na
nchi za Burundi, Rwanda na Uganda ili kuwajengea wananchi uwezo wa kutumia
fursa za kiuchumi.
No comments:
Post a Comment