Na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imesema kuwa nguvu ya soko pamoja na gharama
nyingine zimechangia kutoshuka kwa bei ya taulo za kike licha ya Serikali
kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika taulo hizo.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akijibu swali la Mbunge wa
Viti Maalum Mhe. Sophia Mwakagenda, alietaka kujua sababu za taulo hizo kupungua
bei wakati Serikali iliondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye taulo
hizo katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, pamoja na Serikali kuchukua
hatua ya kuondoa kodi za taulo hizo, imebainika kuwa hakuna mabadiliko ya bei
katika soko jambo linalodhihirisha kuwa bei inaamuliwa na nguvu ya soko
pamoja na gharama nyingine za uzalishaji na uendeshaji.
"Hatua ya kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye
taulo za kike (pads) ililenga kupunguza sehemu ya gharama za uzalishaji wa
bidhaa na kwamba athari chanya ilitotegemewa ilikuwa ni kushuka kwa bei ya
bidhaa hiyo lakini hadi sasa hakuna mabadiliko ya bei katika soko" alisema
Dkt. Kijaji
Alisema kuwa hali hiyo inatokana na sababu mbalimbali
ikiwemo gharama za malighafi, mishahara, uwekezaji, mifumo ya uzalishaji,
teknolojia, ushindani katika soko, umeme, maji safi na maji taka, usambazaji na
ubora wa bidhaa.
"Hivyo basi, kutoshuka kwa kwa bei ya taulo za kike
kunabainisha kuwa kodi inachangua sehemu ndogo sana katika kupanga bei ya
bidhaa, kama ambavyo Serikali imekuwa ikisisitiza na kutoa ufafanuzi mbele ya
Bunge lako Tukufu”, alifafanua Dkt. Kijaji.
Alisema Serikali ina mpango wa kutoa taulo za kike bure ili kuondoa changamoto ya bei ya taulo hizo
inayolalamikiwa kutoshuka na kuwataka wabunge kutolichukulia suala hilo la
upatikanaji wa bidhaa hizo kisiasa kwani hata baadhi ya nchi zilizoondoa kodi
kama hizo ikiwemo Botswana na Kenya, zoezi hili halikusaidia kushusha bei za taulo
hizo.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, kwa sasa mfumo wa uchumi ni wa
soko huria na bei ya bidhaa huamuliwa na nguvu ya soko, yaani ugavi na mahitaji
ya soko, hivyo fursa iliyopo ni kuhamasisha uwekezaji mkubwa kwa kutumia
teknolojia yenye gharama nafuu katika kutengeneza taulo hizo, jambo
linalotakiwa kwenda sambamba na kuchochea ushindani wa bei katika soko na
sio Serikali kuondoa kodi na kupanga bei ya bidhaa.
Serikali ilichukua hatua ya kuondoa kodi ya Ongezeko la
Thamani kwenye taulo za Kike ikiwa na lengo la kupunguza sehemu ya gharama za
uzalishaji wa bidhaa na hivyo kushuka kwa bei, lengo ambalo halijafikiwa.
No comments:
Post a Comment