Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja Biashara
kutoka Shirika la AFRIpads Bi. Liz McNeil wakati wa maadhimisho ya Siku ya
Hedhi Salama Duniani jijini Dodoma.
Na WAMJW-Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameahidi
kuweka masuala ya hedhi salama kwenye Sera
mpya ya Afya ambayo iko mbioni kukamilika ili kuona kama hedhi salama imewekwa
kama kipaumbele.
Ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati wa
kilele cha maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama Duniani ambayo kitaifa
yamefanyika jijini hapa.
Waziri Ummy amesema masuala ya hedhi salama
katika jamii hususan watoto wasichana na wanawake ni muhimu katika kuweka hali
ya usafi wa mazingira rafiki ambapo katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania
inakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama, vyoo bora hasa
mashuleni na sehemu za kazi vyenye chumba cha kubadilishia wakati wa hedhi.
“Katika ripoti za UNICEF na WHO ya mwaka
2013 zinasema kuwa katika kila msichana mmoja kati ya kumi kusini mwa jangwa la sahara anakosa
kwenda shule kwa siku tatu hadi tano kwa sababu ya kuwa kwenye siku za
hedhi”,Alisema Waziri Ummy.
Hata hivyo alisema asilimia 52 ya vyoo vya
wasichana mashuleni havina milango na ni asilimia 1 tu ya shule zimetenga
chumba maalum kwa ajili ya wasichana kujisitiri wakiwa kwenye hedhi kikiwa na
maji na vifaa vya hedhi.
Aidha, aliwataka wadau kuweka mkazo kwenye
kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuzingatia upunguzaji wa bei kwani taulo za
hedhi si bidhaa ya anasa ila ni bidhaa
muhimu kwa mstakabali wa afya na maendeleo ya wanawake na wasichana nchini.
Waziri Ummy ametoa rai kwa wadau wote wa
hedhi salama kutenga fedha kwa ajili ya kujenga walau choo kimoja cha mfano
katika halmashauri kwani jamii ipo
tayari kuchangia maendeleo. Aidha, amekusudia
kila taulo za kike zikatazoingizwa au kuzalishwa Tanzania ziwe na idadi
maalumu za katika kila paketi angalau
taulo kumi.
No comments:
Post a Comment