Na Janeth Jovin
UPANDE wa mashtaka katika kesi ya kumteka nyara Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji maarifu MO inayomkabili dereva Taksi na Mkazi wa Tegeta , Mousa Twaleb (46), umedai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Wakili wa Serikali Dais Makakala alidai leo katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 25 mwaka huu na mshtakiwa amerudishwa rumande.
Twaleb akikabiliwa na mashitaka matatu ikiwemo kumteka nyara Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji maarufu MO.
Katika mashitaka ya kwanza kuwa mshitakiwa alijihusisha na genge la uhalifu.
Inadaiwa Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, mwaka huo huo, katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg Afrika Kusini, kwa makusudi alitoa msaada wa kutendeka vitendo vya jinai au uhalifu wa kupangwa kwa lengo la kujipatia faida.
Pia inadaiwa Oktoba 11, mwaka jana maeneo Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni Dar es Salaam, pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara MO kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.
Pia inadaiwa Julai 10, mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha ambazo ni Sh.8,000,000 wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.
MO alitekwa nyara Oktoba 11, mwaka jana alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika eneo la Gymkhana.
No comments:
Post a Comment