Ofisa Misitu Mkuu wa Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na
Utalii, Seleboni John, akielezea mikakati ya Wizara hiyo katika
kuendeleza misitu kwa maofisa serikali kutoka wilaya mbalimbali katika
warsha iliyoandaliwa na Shirika la Uhifadhi Misitu ya Asili Tanzania
(TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi Misitu Tanzania (Mjumita) na
Shirika la Kuendeleza Nishati ya Asili Tanzania (TaTEDO). (Picha na
Suleiman Msuya).
Ofisa Misitu Mkuu wa Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na
Utalii, Seleboni John akielezea mikakati ya Wizara hiyo katika
kuendeleza misitu kwa maofisa serikali.
Na Suleiman Msuya
UTAFITI
uliofanywa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), chini
ya ufadhili wa Mfuko wa Critical Ecosystem Partnership (CEPF) umebaini
kuwa asilimia 89 ya upotevu wa misitu nchini unachangiwa na shughuli za
kilimo.
Matokeo ya
utafiti huo yametolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo
wakati akiwasilisha mada kuhusu sababu zinachangia upotevu wa misitu
nchini kwa maofisa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) na Serikali Kuu waliokutana mkoani Morogoro.
Lyimo
alisema katika utafiti huo walishirikisha maeneo 120 katika wilaya 62
na mikoa 22 ambapo kila mahali kilimo kilionekana ni sehemu ya sababu
kubwa ya upotevu wa misitu.
"Tumetumia
miezi sita kuzunguka katika wilaya 62 mikoa 22 na maeneo 120 kuangalia
kinachopelekea upotevu wa misitu na tumebaini asilimia 89 hali hiyo
inasababishwa na shughuli za kilimo cha kuhamahama," alisema.
Alisema
utafiti huo umeonesha uvunaji mkaa, uchomaji moto na ufugaji unachangia
upotevu wa misitu kwa asilimia 7, uchomaji moto na ufugaji asilimia 3
na uanzishaji wa mashamba maypa ya miti asilimia 1.
Lyimo
alisema utafiti ulibaini zao ambalo linalimwa zaidi katika maeneo
ambayo misitu imevunwa ni mahindi, ufuta, kunde, mtama, mpunga,
maharage, muhogo, alizeti na korosho.
Alisema
iwapo hali hiyo itaendelea bila kuwepo mipango ya kuendeleza sekta ya
misitu ni wazi rasilimali hiyo itapotea na kukosekana kwa mbao kwenye
vijiji pia kukosekana kwa vyanzo vya maji, uharibifu wa mazingira na
mabadiliko ya tabia nchi.
"Pia
uwezo wa kudhibiti uharibifu utakosekana hasa vijijini hivyo maofisa
wanaohusika na usimamizi wa rasilimali misitu wanatakiwa kuongeza juhudi
kukabiliana na hali hiyo," alisema.
Lyimo
alisema ili maofisa hao kutoka Serikali za mitaa na serikali kuu
kuweza kukabiliana na hali hiyo wanapaswa kuanzisha Usimamizi wa Misitu
ya Jamii (CBFM), jamii kunufaika moja kwa moja na rasilimali misitu na
kuwepo kwa usawa katika maamuzi kuhusu matumizi ya ardhi kwa kushirisha
wadau mbalimbali hasa kilimo, ardhi na misitu.
Kwa
upande wake Ofisa Misitu Mkuu Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya
Maliasili na Utalii, Seleboni John alisema Serikali imejipanga
kikamilifu kusimamia sera ya misitu na sheria ili misitu iwe endelevu.
"Taarifa
zinaonesha uharibifu wa misitu umeongezeka kutokana na kilimo, uchomaji
mkaa na uvunaji wa mbao kinachohitajika ni wadau kushirikiana kudhibiti
kama wanavyofanya TFCG, Mjumita na TaTEDO," alisema.
Mwakilishi
wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Kanda ya Mashariki, Benadetta
Kadala alisema wakala huo umejipanga kulinda misitu kwa kufuata sheria
kanuni.
Aidha, Kadala alisema TFS itahakikisha misitu ya vijiji inakuwa salama na endelevu kwa kusimamia uvunaji wa sheria.
Ofisa
Misitu wa Mkoa wa Morogoro Joseph Chuwa alisema utafiti huo umeonesha
hali halisi ya uharibifu hivyo wao kama maofisa misitu, maliasili,
kilimo, ardhi na sheria hawana budi kujipanga upya kukabiliana na hali
hiyo.
Chuwa alisema iwapo
wao wataongeza jitihada ya usimamizi katika kulinda misitu ni dhahiri
wafanya maamuzi wataungana nao kwenye kampeni hiyo.
No comments:
Post a Comment