HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 11, 2019

KISENA, WENZAKE WARUDISHWA RUMANDE

Robert Kisena.

Na Janeth Jovin
UPANDE wa Jamhuri  katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (UDART), Robert Kisena (46) na wenzake wanne umedai kuwa upelelezi wa shauri bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali Ester Martine alidai leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  jijini Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizire kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelelezi bado haujakamilka hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Rwizire aliahirisha kesi hiyo hadi June 24 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Washtakiwa wamerudishwa rumande.

Mbali na Kisena washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mkewe Frolencia Membe, Kulwa Kisena (33), Charles Newe (47) na raia wa China, Cheni Shi (32).

Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na  mashtaka 19 ikiwemo kusababisha hasara kwa UDART ya Sh. Bilion.2.41.

Katika mashtaka hayo yapo ya Kuongoza genge la uhalifu, kujenga kituo cha mafuta bila kibali, kuuza mafuta sehemu zisizoruhusiwa, Wizi wa mafuta na  utakatishaji fedha wa Sh. Bilioni.1.2, kughushi na kusababisha hasara ya Bilioni.1.4.

Katika shtaka la pili linawakabili washitakiwa wanne ambao ni Kisena, Kulwa, Simon na Florencia ambalo ni kujenga kituo cha mafuta ya petroli bila kibali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)

Katika shitaka la tatu washitakiwa hao inadaiwa kwa kipindi hicho wakiwa wakurugenzi walifanya biashara eneo ambalo halijarusiwa kujengwa.

Katika kosa la utakatishaji fedha linalomkabili Robert Kisena na Chen Shi, Wakili Mwenda alidai kuwa Aprili 8,  2016 katika benki ya NMB Kisena akiwa Mkurugenzi wa UDART alihamisha Sh.Milioni 594.92 kwenda kwenye akaunti nyingine ya Kampuni ya Longway Engineering Company wakati akijua fedha hizo ni zao haramu lililotokana na makosa ya kughushi.

Pia kosa la kuisababishia UDART hasara linawakabili washitakiwa wote ambapo Wakili Mwenda alidai kuwa kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 2016 wakiwa Dar es Salaam waliisababishia hasara UDART  ya Sh. Bilioni.2.41.

Katika kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu linamkabili Kisena na Shi ambapo wanadaiwa walilitenda June 9, 2016 katika tawi la NMB Ilala ambapo kwa nia hovu waijipatia Milioni 603.25 kutoka UDART kwa kuonyesha kiwango hicho kimelipwa kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa  Kituo cha UDART Kimara, Ferry  (Kivukoni), Ubungo na Morocco.

No comments:

Post a Comment

Pages