*Wananchi washangilia, waishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma
Ruangwa, Tanzania
CHANGAMOTO
ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama iliyokuwa inawakabili
wananchi wa vijiji vya Nandagala ‘B’ na Ingawali wilayani Ruangwa
imekuwa historia baada ya Ubalozi wa Uturiki kupitia taasisi yake ya
Diyanet kuwachimbia visima virefu.
Visima
hivyo viwili vimekabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana
(Jumatatu, Juni 3, 2019) na Muambata wa Ubalozi wa Uturuki
anayeshughulikia masuala ya jamii nchini, Muhammed Cicek. Hafla hiyo
imefanyika katika kijiji cha Nandagala ‘B’.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania na Uturuki ni nchi
rafiki na kwamba Serikali ya Uturuki imekuwa ikishirikiana na Serikali
ya Tanzania katika uboreshaji wa huduma za jamii zikiwemo za afya, elimu
na maji.
Waziri
Mkuu baada ya kuvipokea visima hivyo amewataka wananchi wa vijiji hivyo
kupitia kamati zao za maji zihakikishe zinaisimamia vizuri miradi hiyo
na pia wawe wanatoa taarifa za mapato na matumizi ya kila mwezi.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
wilaya ya Ruangwa, Samwel Pyuza ahakikishe huduma ya umeme inafikishwa
katika mradi huo kwa ajili ya kusukuma maji badala ya kutumia jenereta.
Kwa upande wake,
Muambata wa Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala za jamii
nchini, Muhammed Cicek amesema Watanzania na Waturuki ni ndugu, hivyo
amefurahi baada ya wananchi wa vijiji hivyo kupokea zawadi ya visima
hivyo walivyowakabidhi.
Wakizungumza
baada ya makabidhiano hayo, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nandagala
‘B’ wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.
John Magufuli kwa kuwasogezea huduma ya maji karibu na makazi yao.
Mmoja
wa wakazi hao Safina Angulupele (63) amesema awali kabla ya kisima
hicho walikuwa wanapata maji kutoka katika kijiji kingine na pia
hayakuwa na uhakika, hivyo uwepo wa kisima kwenye kijiji chao ni
mkombozi kwao.
Naye
mkazi mwingine wa kijiji hicho Zainab Issa amesema huduma ya maji safi
na salama ni muhimu kwa maendeleo ya jamii, hivyo anaipongeza Serikali
kwa kuwafikishia huduma karibu na makazi. “Sasa hata sisi wazee tunaweza
kwenda kisimani na kuchota maji.”
Serikali
ya Awamu ya Tano kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua
mama ndoo, imedhamiria kuwafikishia wananchi wote huduma ya maji safi na
salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wazee baada ya kuhutubia
mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mandawa wilayani Ruangwa, Juni 3,
2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wazee baada ya kuhutubia
mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mandawa wilayani Ruangwa, Juni 3,
2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua maji baada
ya kukabidhiwa kisima cha maji cha kijiji cha Nandagala ‘B’ kilichojengwa kwa
ufadhili wa Ubalozi wa Uturuki nchini Juni 3, 2019. Kulia ni Muambata wa
Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala ya jamii nchini, Muhammed Cicek na
kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Turkish Maarif Foundation, Oguz Hamza Yilmaz. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment