HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 09, 2019

MGOGORO TEGETA MAGEREJI WAFUKUTA


Paul Makonda - Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu


WANACHAMA zaidi ya 100 wa Tegeta Magereji Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wameamua kukusanya saini kwa ajili ya kuuondoa uongozi uliopo madaraka.

Oktoba 28, mwaka 2016 serikali ilifanikisha kuzirudisha hekari 18 za eneo la Tegeta Magereji Jijini Dar es Salaam kati ya hekari 32 ambazo zilikuwa zikimilikiwa na mwekezajii ikiwa ni jitihada za kutatua mgogoro wa ardhi wa eneo hilo uliodumu kwa muda mrefu.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi waliamua kuzirejesha hekari hizo baada ya vikao kadhaa vya majadiliano baina ya mwekezaji na serikali na kumuomba agawe sehemu ya eneo hilo kufuatia jitihada za awali za kulirejesha eneo hilo kupitia mahakama kugonga mwamba.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baadhi ya wanachama hao walisema kuwa, wameamua kufikia uamuzi huo baada ya kubaini uongozi huo kushindwa kusimamia makubaliano yaliyofikiwa kuhusu mgogoro huo.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama ambao ni Mafundi, Jemset Kandu alisema, hadi sasa wamekusanya saini zaidi 100 na kuutaka uongozi uliopo madaraka kujiuzulu kutokana na kuvunja Katiba ya Umoja huo pamoja na kushindwa kufuatilia kwa miaka mitatu makubaliano yaliyofikiwa kuhusu mgogoro huo.

"Viongozi wetu wanatuhujumu ndiyo maana tumeamua kufikia maamuzi hayo, mbali na kushindwa kufuatilia makubaliano hayo lakini hadi sasa wameshindwa kuwasilisha ada ya usajili Wizara ya Mambo ya Ndani hatua inayotupa hofu ya kufutiwa usajili." alisema.

Alisema kuwa kitendo cha uongozi huo kushindwa kufuatilia makubaliano ya mgogoro huo ili kupata hati kama alivyosema Makonda ni wazi uongozi unahujumu makubaliano hayo.

Naye fundi Ramso Yusub alisema, kutokana na hali hiyo wameamua kuunda Kamati ndogo kwa ajili ya kufuatilia makubaliano yaliyofikiwa ya utatuzi wa mgogoro huo ili kuhakikisha wanapata haki yao ya kumiliki eneo hilo.

Alisema kuwa, kuna hatari ya kuibuka kwa mgogoro kutoka na uongozi kuwagawa wanachama huku wakivunja mkutano ulioitishwa wiki mbili zilizopita baada ya wanachama kuubana uongozi huo kwa maswali yaliyokosa majibu.

"Baada ya miaka mitatu kupita bila kuitishwa kwa mikutano wala kusomwa kwa mapato na matumizi kwa mujibu wa Katiba, Wiki mbili zilizopita uongozi uliita mkutano,

...huku ajenda ikiwa ni moja tu jambo lililosababisha wanachama kuhoji kuhusu ajenda nyingine ikiwemo ya makubaliano yaliyofikiwa kuhusu mgogoro, suala hilo liliwakera viongozi hivyo wakaamua kuvunja mkutano," alisema.

Alisema hivi sasa mafundi wanalia kwa kukosa mapato baada ya wateja kushindwa kuingiza magari katika gereji ya umoja huo kutokana na barabara kutopitika kirahisi.

Akizungumzia madai hayo, Katibu wa Umoja wa Magereji, Munir Ramadhan alisema kuwa hana taarifa kuhusiana na mkutano huo bali anachodhani ni uwepo wa baadhi ya watu wanaotaka kuvuruga Umoja huo.

Alisema kuwa wanazotaarifa za kuwepo kwa baadhi ya wanachama wanaotaka kuvuruga Umoja huo ambao wamekuwa walikusanya saini hizo.

" Nikuombe kesho (leo) ufike magereji ili niweze kuonana nawe na tuongee wazi wazi kuhusu wapi tulipofika kama uongozi katika kushughulikia mgogoro huu, " alisema Katibu huyo.

Baada ya kutatuliwa kwa mgogoro huo wananchi hao walitakiwa kusubiri hati ya eneo hilo ambayo ilipaswa kutoka ndani ya wiki mbili tangu kutatuliwa kwa mgogoro huo ili kuitumia hati hiyo kwa ajili ya matumizi mengine ikiwemo kuombea mikopo.

No comments:

Post a Comment

Pages