Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Maji Zanzibar {ZAWA} Nd, Mussa Ramadhan akimpatia maelezo Balozi Seif hatua zinazochukuliuwa na Mamlaka hiyo katika
kuona Mradi wa ujenzi wa Tangi la Maji unazingatia Vigezo vyote.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifanya ziara ya kukagua eneo linalotarajiwa
kujengwa Tangi kubwa na la Kisasa la Maji safi na salama la ujezo wa Lita Laki
1.5 katika Kijiji cha Kitope ndani ya Jimbo la Kiwengwa.
Balozi Seif akiupongeza Uongozi
wa Jimbo la Kiwengwa kwa jitihada unazochukuwa za katika usimamizi wa kuondosha
changamoto zinazowakabili Wananchi wao. Picha na – OMPR – ZNZ.
Unguja, Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi ameziomba na kuzikumbusha Taasisi na Makampuni yanayojitolea kusaidia
huduma za Kijamii nchini kuzingatia mahitaji halisi ya Wananchi ili misaada pamoja
na Miradi wanayoigharimia iweze kukidhi vigezo sahihi.
Alisema ipo miradi kadhaa ya wananchi akatolea mfano
huduma za maji safi na salama inayopata nguvu za Uwezeshaji moja kwa moja
kutoka kwa Taasisi Wahisani inapaswa kwenda sambamba na ukuaji wa maeneo hasa
Miji Midogo iliyopo Wilayani na Mikoani inayotokana na ongezeko la Idadi ya
Wakaazi wake.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo alipofanya
ziara fupi ya kukagua eneo linalotarajiwa kujengwa Tangi Jipya na la Kisasa
katika Mtaa wa Kitope baada ya lile liliopo kuachakaa na kushindwa kukidhi
mahitaji halisi ya sasa kutokana na kuongezeka kwa Idadi ya Watu.
Ziara hiyo pia ilikwenda sambamba na kukagua ujenzi
wa Mnara utakaokuwa na uwezo wa kuhifadhi Maji katika Matangi Mawili yenye ujazo
wa Lita Elfu kumi kila Moja katika
Kijiji cha Kitope Muembe Majogoo ndani ya Jimbo la Kiwengwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema umuhimu
wa Huduma za Maji safi na Salama unaeleweka na kila Mwana Jamii suala ambalo
ipo haja kwa washirika wenye uwezo na Taaluma kulitia maanani jambo hilo katika
kuona changamoto zinazowakabili Wananchi katika kupata huduma hiyo linaondoka.
Balozi Seif aliwapongeza
Viongozi kuanzia Wadi hadi Jimbo la Kiwengwa kwa jitihada wanazoendelea
kuzichukuwa katika kusimamia mapambano dhidi ya changamoto mbali mbali
zinazowakabili Wananchi wao.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Nd. Mussa Ramadhan alisema upo mpango wa hivi karibuni wenye muelekeo wa
kujenga Tangi jengine jipya la kuhifadhia Maji safi na salama katika eneo la
Kitope.
Nd. Mussa alisema ujenzi wa Tangi hilo litakalokuwa
na ujazo wa lita Laki Moja na Nusu chini ya ufadhili wa Washirika wa Maendeleo
umekuja kufuatia lile la asili kuchakaa pamoja na ujazo mdogo wa Lita 50,000
ambapo kwa sasa mahitaji ya huduma hiyo yameongezeka kutokana na kukua kwa
Vitongoji.
Alisema Mamlaka ya Maji Zanzibar ikiwa msimamizi na
mshauri muelekezi wa Ujenzi wa Mradi huo wa Tangi la Maji tayari imeshatoa
michoro na harakati za kumpata mjenzi wa Tangi hilo ndani ya kipindi cha Miezi
Miwili kuanzia sasa umeanza.
Naye Diwani wa Wadi wa Mbaleni Ndugu Hassan Ameir
Abdulla alisema Ujenzi wa Mnara wa
kuhifadhia Matangi ya Maji Mawili yenye Ujazo wa Lita Elfu Kumi Kila Moja uko
katika hatua nzuri kwa lengo la kuwaondoshea tatizo la Huduma hiyo inayowasumbua
kwa muda mrefu sasa.
Nd. Hassan alimueleza Balozi Seif kwamba Mradi huo
unaokisiwa kugharimu zaidi ya shilingi Milioni 35,000,000/- za Kitanzania
unatarajiwa kukamilika rasmi kabla ya Mwezi wa Nane Mwaka huu.
Diwani huyo wa Wadi wa Mbaleni aliahidi kwa
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar aliyekuwepo kwenye ziara hiyo kwamba
Timu yao itakuwa tayari kushirikiana na Wahandisi wa Mamlaka ya Maji katika
kuona Mradi huo unafanikiwa vyema katika kiwango kinachokubalika Kitaalamu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
09/06/2019.
No comments:
Post a Comment