HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 11, 2019

RAIS MAGUFULI AIPAISHA SEKTA YA AFYA MARADUFU


Na Dotto Mwaibale, Dodoma

MKUU wa Wilaya ya Dodoma mjini, Patrobass Katambi, amesema Rais Dkt.John Pombe Magufuli ameipaisha sekta ya afya maradufu kwa kutenga bajeti kubwa ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara tangu aingie madarakani.

Katambi aliyasema hayo wakati akizungumza na maofisa wa Bohari ya Dawa (MSD) waliopo mkoani Dodoma kutembelea wateja wao ili kujua changamoto zilizopo ili zitafutiwe ufumbuzi baada ya MSD kufanya maboresho makubwa ya upatikanaji wa dawa nchini.

"Kwa kweli Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wamefanya kazi kubwa ya upatikanaji wa dawa, ujenzi wa vituo vya afya vya kisasa na maboresho mbalimbali katika sekta hiyo" alisema Katambi.

Alisema baada ya vituo hivyo vya afya kuboreshwa miundombinu yake na kujengwa vingine vimekuwa kama Hospitali za wilaya za miaka ya nyuma.

Alisema Dodoma hivi sasa kuna Hospitali kubwa mbili ya Benjaminil Mkapa na ya General na zote zinatoa huduma nzuri bila ya kuwepo malalamiko yoyote.

Katambi alisema Rais Dkt. John Magufuli baada ya kuona Jiji la Dodoma siku za mbeleni kuja kuwa na ongezeko kubwa la watu alitoa sh milioni 950 ambazo zilikuwa zitumike katika sherehe ya Maadhimisho ya Sikukuu ya Uhuru ili ijengwe Hospitali kubwa itakayoitwa Uhuru itakayojengwa Chamwino.

Aliongeza kuwa katika Jiji la Dodoma hakuna tena changamoto ya ukosekanaji wa dawa na vifaa tiba na hiyo imetokana na ubunifu, mifumo ya kisasa na mapinduzi makubwa ya kiutendaji yaliyofanywa na MSD.

Alisema kazi inayofanywa hivi sasa na MSD ni ya kimataifa kwani wana magari ya kutosha ya usambazaji wa dawa nchi nzima, wafanyakazi wake wapo nadhifu wakati wote na dawa zinawafikia walengwa kwa wakati jambo linalo wafanya wananchi kuwa na imani na MSD.

No comments:

Post a Comment

Pages