Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki, kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngoro Malenya na kulia kwa Naibu Waziri ni Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini Stela Tulo. (Picha na Hassan Mabuye- WIZARA YA
ARDHI).
Na Munir Shemweta, WANMM ULANGA
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amepiga marufuku wananchi
wanaoshitakiana katika Mabaraza ya Ardhi kutoa pesa kwa ajili ya kugharimia
usafiri wa kwenda eneo lenye mgogoro.
Akizungumza wakati wa
kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro mwishoni
mwa wiki Dkt Mabula alisema, kutoa pesa ya kugharamia usafiri kwa mmoja wa wanaoshitakiana
katika Mabaraza ya Ardhi kwenda eneo la tukio kunaweza kuleta ushawishi kwa
wajumbe wake hasa kwa yule aliyetoa kiasi kikubwa cha pesa.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi alisema, ni lazima wakati wa zoezi la kwenda eneo lenye
mgogoro kwa wanaoshitakiana katika Mabaraza ya Ardhi Mkurugenzi wa Halmashauri
husika aratibu zoezi hilo huku ratiba nzima ikiwasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya katika
kipindi cha mwezi mmoja.
‘’ Jamaa anatoa laki
mbili anayelalamika hana kitu unategemea hapo haki itatendekaje, ni marufuku kabisa
na taratibu zote za kwenda uwandani zipitie kwa DC na ratiba ijulikane mapema’’
alisema Dkt Mabula.
Akigeukia uzinduzi wa
Baraza la Ardhi na Nyumba katika wilaya ya Ulanga, Dkt Mabula alisema Serikali
imezindua Baraza hilo ili kupeleka
huduma karibu na kurahisisha usikilizaji kesi za ardhi kwa wananchi ambao baadhi ya maeneo
wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kupata huduma hiyo na kubainisha kuwa sasa
wananchi wa Ulanga watapata haki kwa
wakati na kwa umbali mdogo.
Aliwaasa wananchi wa wilaya
ya Ulanga kulitumia vyema Baraza Ardhi na Nyumba lililozinduliwa na kuwataka kuhakikisha
wanafuata taratibu zote za utatuzi wa migogoro ya ardhi pamoja na kuachana na ile
migogoro ya kifamilia kwa kutumia Mabaraza ya Vijiji na Kata kushughulikia
migogoro hiyo.
Dkt Mabula aliusifu
mkoa wa Morogoro kwa kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na kubainisha
kuwa mafunzo hayo yawe chachu kwa wajumbe wake kutenda haki wakati wa kufanya
maamuzi kwa kuwa tayari wana weledi katika eneo hilo.
Kwa upande wake Msajili
wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini Stela Tulo alisema, uzinduzi wa Barazala
la Ardhi katika wilaya ya Ulanga limejibu kiu ya muda mrefu ya wananchi wa wilaya
hiyo kupata huduma kwa ukaribu ambapo awali iliwalazimu kusafiri umbali mrefu hadi
Kilombero kupata huduma.
Kwa mujibu wa Stela,
kuzinduliwa kwa Baraza la Ulanga sasa kunaufanya mkoa mzima wa Morogoro kuwa na
Mabaraza ya Ardhi na Nyumba Manne (4) na kubainisha kuwa Baraza hilo sasa
linaongeza idadi ya Mabaraza yanayofanya kazi nchini kufikia 54 kati ya 97
yaliyoidhinishwa.
Msajili huyo wa
Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini alisema, mkoa wa Morogoro pekee kwa sasa una
Mashauri 2,500 ya ardhi kati ya 29,000 nchi nzima na kubainisha kuwa,
kuzinduliwa kwa Baraza la Ulanga ni moja ya jitihada kuhakikisha Mashauri
katika mkoa huo yanapungua kama siyo kuisha kabisa.
No comments:
Post a Comment