Waziri wa Elimu na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akikata utepe kuzindua Mabaraza ya Ujuzi ya Kiseta jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wadau kutoka sekta za uchumi hapa nchini wamepongeza hatua ya Serikali na taasisi ya Sekta Binafsi kuanzisha mabaraza ya kisekta ya ujuzi kwani hiyo ni ishara njema kwa ujenzi wa sekta ya viwanda.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki, wadau wamesema hatua ya kuanzisha mabaraza hayo ni chanya na itawasaidia wahitimu kuwa na uwezo wa kujiamini na kutoa mchango mkubwa wanapokuwa katika ajira.
Mkuu wa Chuo cha Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Preksedis Ndomba amesema, kuanzishwa kwa mabaraza hayo ni fursa pekee kwa chuo chake kunufaika na huduma ya mabaraza hayo.
“Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kushirikiana bega kwa began a sekta binafsi imeonyesha njia, hivyo ni jukumu la wadau kutoka sekta mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo ili kutimiza azma ya Serikali ya viwanda ifikapo 2025m,’’ alisema.
Naye mdau mwekezaji wa ndani katika sekta ya nishati mbadala, Bwana Hilary Biduga alisema yeye kama mwekezaji anahitaji wafanyakazi wenye ujuzi ili kufanikisha azma yake, hivyo mabara hayo yatachochea ukuaji na maendeleo ya sekta mbalimbali.
“Nikiwa kama mdau wa maendeleo na mwekezaji wa ndani, hatua iliyofikiwa na Serikali na Sekta binafsi kuanzisha mabaraza ina lengo jema kwa nchi, kwani kupitia mabaraza haya vijina wataleta ushindanikatika soko la ajira,’’ alisema Bwana Biduga.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Bwana Godfrey Simbeye amesema TPSF kama msimamizi na mratibu mkuu wa mabaraza hayo watahakikisha malengo ya kuanzishwa kwa mabaraza hayo yanatekelezwa kama ilivyokusudiwa.
“Mabaraza haya ndiyo daraja la kuwavusha vijana kuelekea katika fursa mbalimbali hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kufikia azma ya serikali ya kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025,’’ alisisitiza.
Aidha Bwana Simbeye amepongeza ushirikiano uliopo kati ya sekta binafsi na serikali katika kutimiza azma ya kuanzishwa kwa mabaraza. “Niipongeze serikali na TPSF kwa kuafikiana na hatimaye kuanzishwa kwa mabaraza ambapo inaonyesha ishara nzuri ya kiushirikiano kati ya serikali na TPSF katika kutatua changamoto mbalimbali ili kuendelea kuwa na mazingira mazuri ya kibiashara, uchumi na uwekezaji,’’ alisema.
Akizungumza zaidi kuhusu mabaraza, Bwana Simbeye amesema elimu zaidi itatolewa nchi nzima kuhusiana na umuhimu wa mabaraza hayo na namna TPSF ilivyojipanga kufanikisha utekelezaji ikiwemo kuwawezesha vijana wanaomaliza vyuo vya kati na vikuu kuingia kwenye ushindani wa soko la ajira ndani na kimataifa. Bwana Simbeye ambaye ni muumini mkubwa wa majadiliano kama sehemu pekee inayoweza kuzikutanisha sekta za umma na binafsi na kufanya kazi pamoja na kuleta matokeo chanya kwa mustakabali wa Taifa.
No comments:
Post a Comment