Na Mwandishi Wetu
WANANCHI kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es
Salaam wameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kitendo cha kutoa huduma
za upimaji wa afya bure katika kuadhimisha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa
Umma ambayo yanahitimishwa leo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wamesema kuwa suala la
afya ni suala muhimu kwa maisha ya wananchi lakini pia ili mwananchi yoyote
aweze kuchangia pato la familia na Taifa ni lazima awe na afya njema hivyo
kitendo cha kutoa elimu ya afya kwa wananchi ni kitendo kikubwa na kupigiwa
mfano.
“Kitendo cha kujua hali ya afya yako kama mwananchi
kinakupa nguvu ya kupanga mipango yako ya maendeleo, suala la afya ni suala
nyeti sana kwa kuwa hakuna mtu yoyote anayeweza kushiriki shughuli za maendeleo
akiwa na afya mbovu, nawapongeza sana NHIF kwa kuweka huduma hizi tena bure
imetusaidia sana ambao tumepata huduma hii,” alisema Bw. Mohamed Shitindula
Mkazi wa Mwananyamala.
Mfuko ulianza kutoa huduma hizo tangu Juni 16 hadi Juni
23, mwaka huu katika viwanja vya Ofisi yake ya Mkoa wa Kinondoni iliyopo,
Mwenge njia ya kuelekea Coka Cola.
Mwananchi mwingine ambaye pia ni Mwanachama wa NHIF, Bw.
Fanuel Msangi alisema kuwa huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni mkombozi
wa majanga ya magonjwa ambayo yanaweza kuwapata wananchi wakati wowote hivyo
akawaomba kujiunga na Mfuko ili kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati
wowote.
“Ukiwa na kadi ya NHIF unakuwa na uhakika wa matibabu
mahali popote unapokuwa, kwa mfano mimi kupitia uanachama wangu familia yangu
inahudumiwa pamoja na wazazi wangu hivyo nimeona faida kubwa ya kuwa ndani ya
huduma za Mfuko na nitumia fursa hii kuwapongeza kwa maboresho makubwa ambayo
wameyafanya katika huduma zao,” alisema Bw. Msangi.
Kwa upande wake Meneja wa NHIF, Kinondoni Bw. Innocent
Mauki, alisema kuwa, Mfuko umetoa huduma za upimaji wa afya bure ili kuwezesha
wananchi wengi zaidi kupata huduma hizo na kufahamu hali ya afya zao pamoja na
elimu itakayowawezesha kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
“Katika Wiki hii ambayo Mfuko tuliamua kudhimisha Wiki
ya Utumishi wa Umma kwa kutoa huduma kwa wananchi, tumefarijika kuona mwamko
mkubwa wa wananchi umejitokeza na kupima afya pamoja na kupata elimu ya huduma
za bima ya afya. Nitoe rai tu kwa wananchi wote ambao wako nje ya Mfumo wa bima
kujiunga na huduma hizi kwa kuwa magonjwa huja bila taarifa na Mfuko umejiandaa
kuhakikisha unatoa huduma bora kwa wanachama wake,” alisema Bw. Mauki.
Alisema kuwa mbali na huduma hizo ambazo zimetolewa Mkoa
wa Dar es Salaam, Mfuko kupitia Ofisi za Mikoa zilitumia fursa hii kutembelea
Vituo vya kutolea huduma kwa lengo la kuona huduma wanazopata wanachama wake na
kupata mrejesho kutoka kwao.
No comments:
Post a Comment