Baadhi ya
watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakiwa kwenye picha ya pamoja
baada ya kufanya usafi wa mazingira kwenye Hospitali ya Rufaa ya Wagonjwa wa
Akili ya Mirembe, iliyopo mkoani Dodoma.
Baadhi ya
watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakiendelea kufanya usafi wa
mazingiea kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mirembe, mkoani Dodoma.
Na Mwandishi
Wetu, MOHA
UONGOZI wa
Hospitali ya Rufaa ya Wagonjwa wa Akili ya Mirembe, mkoani Dodoma, umefurahishwa
na kitendo cha watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwenda kufanya
usafi wa mazingira hospitalini hapo.
Pongezi hizo
zimetolewa na Kaimu Mganda Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Escor Tweve.
Watumishi
hao wakiwa na baadhi ya viongozi wa Wizara, idara zilizopo chini ya Wizara
hiyo, waliadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kufanya usafi wa mazingira
hospitalini hapo.
“Nawashukuru
kwa uamuzi wa kuja kufanya usafi wa mazingira hospitalini hapa kwa kufyeka,
kulima, kuchoma taka, kudeki na kufanya kazi nyingine za kijamii.
“Mmeonyesha
upendo mkubwa mlionao dhidi yetu, mmejitoa kwa moyo wa dhati, miaka mingi
imepita hatujawahi kupata ugeni uliofanya jambo muhimu kama hili,” alisema Dkt.
Tweve.
Mbali ya
kufanya usafi wa mazingira, watumishi hao walipata fursa ya kupewa elimu juu ya
huduma zinazotolewa kwa wagonjwa hospitalini hapo.
Dkt. Tweve
alisema changamoto kubwa waliyonayo wagonjwa wa akili huwa hawapendwi katika
jamii ila ni watu wanaopaswa kupewa upendo mkubwa na jamii.
“Wagonjwa wa
akili hawana tofauti na watu wengine ambao hawana matatizo kama yao kwenye
jamii, wanapoletwa hapa hospitali huwa tunawapatia matibabu, kupona, kutoa
michango mizuri kwenye jamii na nchi kwa ujumla,” alisema.
Aliishukuru
Wizara hiyo kwa ushirikiano mkubwa wanaowapa kwani kuna wagonjwa wengine wa
akili hukamatwa, kuhitajika kufanyiwa matibabu hospitalini hapo.
Pia wapo
baadhi ya watumishi wa idara za serikali wakiwemo askari ambao hospitali hiyo
huwapatia matibabu ya akili, kupona, kuendelea na majukumu yao ya kazi.
“Naishukuru
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuadhimisha siku hii kwa kuja Mirembe na
kufanya usafi wa mazingira, nawaomba muwe na utaratibu wa kuja mara kwa mara,”
alisisitiza.
Aliwapongeza
watumishi wa Wizara hiyo na viongozi wao akiwemo Waziri Kangi Lugola, Naibu
Waziri, Mhandisi Hamad Masauni, Katibu Mkuu, Meja Jenerali Jacob Kingu, Naibu
Karibu Mkuu, Ramadhani kailima kwa utendaji mzuri wa kazi.
Kwa upande
wake, Mkuu wa Kitengo cha TEHAWA katika Wizara hiyo, Jane Massawe ambaye
alimwakilisha Katibu Mkuu, aliushukuru uongozi wa hospitali hiyo kwa ushirikiano
walioutoa kwa watumishi hao.
“Tumefurahishwa
na mapokezi mliyotupa, tupatapo nafasi kwa siku nyingine tutakuja kuwatembelea
na kufanya shughuli za kijamii,” alisema Massawe.
Wiki ya
Utumishi wa umma ilianza huadhimishwa kuanzia Juni 17 hadi 22, mwaka huu.
Maadhimisho hayo ni kwa mujibu wa Kalenda ya Umoja wa Afrika (AU).
Nchi
mbalimbali huadhimisha siku hiyo kwa kushiriki shughuli mbalimbali zinazohusu
utumishi wa umma.
No comments:
Post a Comment