Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Na Asha Mwakyonde
WAZIRI
wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema
anatarajia kupeleka muswada bungeni wa dereva atakayeendesha pikipiki
kabla ya kupewa leseni awe na bima ya afya kwanza.
Alitaja
sababu ya kutaka kupeleka muswada huo bungeni ni kutokana na ajali
zitokanazo na pikipiki kuwa nyingi na kusababisha gharama za matibabu
kwa sekta ya afya kuwa kubwa.
Akizugumza
jijini Dar es Salaam leo, wakati wa ufunguzi wa kambi ya utoaji wa
miguu bandia kwa kwa watu 600 katika taasisi ya Tiba ya Mifupa
Muhimbili (MOI), Waziri Ummy alisema taasisi hiyo kwa mwezi imekuwa
ikipokea wagonjwa 700 hadi 900 wa ajali za pikipiki.
Ummy
alisema idadi hiyo ni kubwa na imekuwa ikiongezeka kila siku kwa sababu
awali taasisi hiyo ilikuwa ikipokea wagonjwa wa ajali hizo 400 hadi 600
kwa mwezi.
“Nimeongea na
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kumuomba waangalie jinsi ya
kuzidhibiti pikipiki hizo kwani zimekuwa zikibeba zaidi ya abiria wawili
hadi watatu,hivyo nimemuomba kabla dereva bodaboda hajapewa leseni
sharti la kwanza awe na bima ya afya ndio apatiwe leseni yake ya
udereva,”alisema.
Alisema
ni vyema kila mtu akawa na bima ya afya kwa sababu gharama za upasuaji
pindi mtu apatapo ajali ni kubwa, Taasisi ya MOI gharama za upasuaji
mdogo ni sh. 200,000 na ili mtu apatiwe mguu ni sh. milioni 1.5 hadi
tatu.
Vilevile Ummy
alisema katika kambi ya upimaji wa watu wanaotakiwa kupatiwa miguu
bandia waliojiandikisha walikuwa 900 na waliofanikiwa kupewa miguu hiyo
ni 600 hivyo aliwaahidi kuangalia namna ya 300 waliobaki kupatiwa miguu
hiyo.
“Zoezi hilo
limefanikiwa kwa kushirikiana na Ubalozi wa China ambao umekuwa mstari
wa mbele kuchangia sekta ya afya ambapo mwaka jana walichangia dawa
zilizokuwa na thamani ya sh.bilioni mbili na wameahidi tena kutoa fedha
hizo mwaka huu ambapo dawa za sh.milioni 500 watapewa MOI,”alisema.
Alisema
ameona dawa za sh.milioni 500 kupewa MOI kwa sababu amekuwa akiridhika
na huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo japo ya kuwa na baadhi ya
changamoto wanazokabiliana nazo.
Hata hivyo aliwaahidi MOI kuwa serikali itahakikisha inatatua changamoto zilizopo kwa wakati.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi wa MOI, Charles Mkonyi, alimshukuri Raisa Dk. John
Magufuli kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma,kufunga vifa vya kisasa vya
uchunguzi.
“Mafanikio ya
MOI, Rais Dk. Magufuli ndio muasisi wa ushirikiano uliopo kati ya
taasisi hiyo na serikali ya China,hivyo tunamuomba Waziri Ummy kusaidia
upanuzi wa eneo la mazoezi kwa sababu kwa sasa kumekuwa na ongezeko
kubwa la wagonjwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment