Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Dk Felix Nandonde ( kushoto) akisisitiza jambo alipokuwa wakifungua wakati mafunzo kwa wachunaji wa ngozi wa machinjio ya ngozi Manispaa ya Morogoro na (kulia) ni Kaimu Mkurugenzi msaidizi wa mazao ya mifugo,usalama wa chakula na lishe kutoka Wizara hiyo, Gabriel Bura , na (kati kati) ni Afisa Mifugo mkoa wa Morogoro,Dk Gasper Msimbe.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya Manispaa ya Morogoro wakimsililiza mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa mafunzo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya Manispaa ya Morogoro wakimsililiza mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa mafunzo.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
SERIKALI kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutoa mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio mbalimbali nchini ili waweze kuboresha kazi zao kwa kutoa mazao bora ya ngozi zitakazo ingiza fedha za kigeni kutokana na mauzo ya nje, na kukuza uchumi wa taifa na kuanzishwa kwa Viwanda vya ngozi.
Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko kutoka Wizara hiyo, Dk Felix Nandonde alisema hayo wakati akifungua mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya Manispaa ya Morogoro.
Dk Nandonde alisema , Tanzania imekuwa ikipata kiasi kidogo cha fedha za kigeni kutokana na uharibifu wa ngozi licha ya kuwa ni nchi ya pili kwa uwingi wa mifugo Barani Afrika baada Ethiopia.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo , kwa sasa Tanzania ina ng’ombe milioni 32.2, mbuzi milioni 20 na kondoo milioni tisa, na kwamba ngozi zote zingeweza kusimamiwa ubora wake na kuingia katika mfumo wa biashara ya ngozi pato la Serikali na Wananchi lingeongezeka kwa kiwango kikubwa.
Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko kutoka Wizara hiyo alisema , kwa sasa asilimia 50 ya uharibifu wa ngozi ikifanyika katika machinjio hasa wakati wa uchunaji.
Dk Nandonde a lisema , kutokana na mapungufu hayo,Wizara imeamua kuja na mkakati mahususi juu ya mbinu mpya ili kuikwamua sekta ndogo ya ngozi ili na kuifanya itoe mchango mkubwa zaidi kwa kuwapa mafunzo maalumu wachunaji wa ngozi katika machinjio.
Hata hivyo alisema , kuwa kwa sasa sekta hiyo ya ngozi imekuwa ikitoa mchango katika pato la Serikali na mtu mmoja mmoja ambapo kwa mwaka 2017/18 jumla ya Sh 5,098,846,623 zilipatikana wakati Sh 5,254,388,808 zilikusanywa na Serikali katika kipindi cha Machi 2018/19 kutokana na kusafirisha ngozi na bidhaa zake nje ya nchi.
Naye Kaimu Mkurugenzi msaidizi wa mazao ya mifugo,usalama wa chakula na lishe kutoka Wizara hiyo, Gabriel Bura alisema ,wameamua kutoa mafunzo hayo kwa Wachunaji ngozi kutokana na sheria ya biashara ya ngozi namba 18 ya mwaka 2008 inawataka kufanya hivyo na kisha baada ya mafunzo watapewa leseni ya uchunaji ngozi na kuweza kutambulika na Serikali.
Alisema kuwa kupitia sheria hiyo ya ngozi mambo mengi yanatakiwa kusimamiwa ikiwemo ya machinjio yoyote wakati wa kusajiliwa kuwepo kwa watalaam wenye mafunzo ya namna ya kuchuna ngozi na ili kuhakikisha ubora wa ngozi unasaidia kuinua sekta ndogo ya ngozi.
Naye Afisa Mifugo mkoa wa Morogoro,Dk Gasper Msimbe alisema, zaidi ya Wachunaji wa ngozi 200 wa Manispaa ya Morogoro watapatiwa mafunzo hayo yenye lengo la kuwapa mbinu mpya za uchunaji ili kuhakikisha wanasaidia kupatikana kwa ngozi yenye ubora.
Mmoja wa wachunaji wa ngozi katika machinjio hiyo ya Manispaa ya Morogoro, Alex Chiboyi alisema, kupitia mafunzo hayo yatawezesha kuzalisha ngozi yenye ubora na kuongeza kipato chao.
Chiboyi ambaye anauzoefu wa miaka 20 katika uchunaji wa ngozi katika machinjio aliishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huo unaoensa sambamba na utoaji wa leseni kwani zitawasaidia kuwepo na usimamizi mzuri na kuondokana na matapeli .
No comments:
Post a Comment