Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Salim Abri, akizungumza wakati wa uzinduzi ofisi ya madereva daladala.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Salim Abri, akiwa katika
picha ya pamoja na madereva daladala wa manispaa ya Iringa. (Picha na Denis Mlowe).
Na Denis Mlowe, Iringa
MWENYEKITI wa Kamati ya Usalama Barabarani mkoa wa Iringa,
Salim Abri, amewataka madereva daladala kuzingatia sheria za usalama
pindi wanapokuwa wakiendesha daladala zao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ofisi mpya ya madereva wa
daladala manispaa ya Iringa, Abri alisema kuwa ifike wakati madereva
wafate sheria kuepukana na usumbufu wa vyombo vya usalama.
Alisema kuwa imekuwa kawaida ya madereva wa daladala
kuvunja sheria kisha kuanza malalamiko kwamba wanaonewa na polisi wa
usalama Barabarani hali ambayo imesababishwa na madereva kutofata
sheria.
Abri ambaye pia ni mkurugenzi wa
kampuni ya usafirishaji ya Asas alisema kuwa kuna baadhi ya madereva
wanaokiuka taratibu za ushafirishaji ikiwemo kutofika mwisho wa vituo
hali inayoleta usumbufu kwa abiria.
Alisema madereva wanapaswa kufata
sheria ikiwemo kutoa tiketi kwa abiria lakini pia kuepuka kuwanyanyasa
abiria kwa kutotumia lugha mbaya kwa abiria ambao wamewapakia.
Aliongeza kuwa licha ya kufata sheria madereva wametakiwa
kuondokana na migomo isiyokuwa na maana kwa lengo la kufikisha kilio
chao katika mamlaka husika kwani kugoma sio njia ya kutatua tatizo.
"Hivi unavyogoma mnajua kwamba wengine wanafurahia Sana
hali hiyo? Kumbukeni kuna njia nyingi za kufikisha ujumbe kwa serikali
endapo mnaona mambo hayapo sawa hivyo acheni tabia ya kugoma" Alisema.
Katika
uzinduzi huo Abri aliwachangia sh. Milioni kumi kwa ajili ya kufungua
Saccos ya madereva daladala na kuwataka kutumia vyema Saccos hiyo katika
kukuza uchumi.
Aliwataka
pia kuacha tabia ya kushabikia mambo ya siasa zisizo na faida kwao
ambazo haziwezi leta maendeleo kisa unafata mkumbo kutoka kwa watu
wengine.
Alisema
kuwa wanatakiwa kuangalia viongozi ambao wapo kwa ajili ya kuwaletea
maendeleo ambayo wanayataka na kukiamini chama cha Mapinduzi chenye nia
haswa ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Kwa
upande wao madereva wa daladala kupitia katibu wao, Rashid Ayubu
waliomba mafunzo ya Mara kwa Mara ikiwezekana kila baada ya miezi Sita
kutokana na mabadiliko ya sheria ya mara kwa mara.
Ayubu
alisema kuwa umoja huo Una mpango wa kupata gari aina ya Kosta kwa
lengo la kuwaongezea kipato lenye thamani ya sh. Milioni 56 na kufungua
Saccos ya umoja huo.
Aidha
alisema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni baadhi ya barabara
zimekuwa chakavu na zinahitajika matengenezo makubwa na nyingine
kushindwa kuendelea na safari kutokana na kuvamiwa na bajaji na
bodaboda.
No comments:
Post a Comment