HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 27, 2019

Mikoa 21 yaathiriwa na Viwavijeshi Vamizi

Mtafiti Kiongozi Dk. Gration Rwegasira, akiwasilisha ripoti ya utafiti kuhusu athari za Viwavijeshi Vamizi kwenye mazao, mkoani Dodoma juzi. (Na Mpiga Picha Wetu).

Na Suleiman Msuya

WATAFI wa Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na wadau wengine wa kilimo wamebaini Viwavijeshi Vamizi vimeathiri mazao katika mikoa 21 nchini.

Utafiti huo umefanywa kwa kipindi cha miezi minne kwa ufadhili wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) ambapo wilaya 42 katika mikoa 21 zilihusika.

Mtafiti Kiongozi kutoka SUA, Dk. Gration Rwegasira alisema wamelazimika kufanya utafiti huo ili kuweza kubaini athari za wadudu hao hatari kwenye kilimo.

Alisema mikoa na wilaya ambazo wamepita athari ni zaidi ya asilimia 80 hivyo nidhahiri kuwa mavuno hayatakuwepo kwa wakulima wa mikoa husika.

Mtafiti huyo alisema jitihada zaidi zinahitajika kukabiliana na viwavijeshi hasa kwa kutoa elimu kwa maofisa ugani na wakulima kuwatambua na kukabiliana nao.

Rwegasira alisema ripoti hiyo ya utafiti amesema usalama wa chakula sio ukubwa wa eneo lililolimwa pekee bali kile kinachovunwa na wakulima ndicho kinachoweza kuonyesha kwamba nchi inajitosheleza kwa chakula.

"Tumezunguka kwa takribani miezi minne kipindi hiki cha kilimo na mavuno hali sio nzuri Viwavijeshi Vamizi vimeharibu mazao kwa zaidi ya asilimia 80 na ukiangalia kwa kina tatizo ni uelewa wa maofisa ugani na wakulima kuhusu kukabiliana na hali hiyo," alisema.

Alisema katika utafiti wao wamebainisha kuwa kuna matumizi makubwa ya madawa ya viwandani yaani viuatilifu katika kumdhibiti mdudu huyu bila mafanikio na hivyo kuhatarisha afya ya wakulima na mazingira.

Aliongeza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa viuatilifu wasio waaminifu wamekuwa wakiwauzia wakulima dawa za kunguni na kwakuwa wakulima hawajui na wapo kwenye taharuki ya kuokoa mazao yao yanateketea wananunua na kwenda kupulizia bila mafanikio.

Dk. Rwegasira alisema wakulima baada ya kuona viuatilifu hivyo havifanyi kazi baadhi wanachanganya kiuatilifu zaidi ya kimoja bila kujua athari za kikemikali za mchanganyiko wa madawa wanayochanganya.

Kiongozi huyo wa utafiti huo kutoka SUA alisema tatizo kubwa linatokana na maafisa ugani wenyewe ambao ndio wanaotakiwa kumshauri mkulima kukosa elimu ya utambuzi na udhibiti wa  mdudu huyo na wala njia bora za kumkabili na hivyo kuendelea kusababisha athari kwenye mashamba ya wakulima.

"Utafiti huo umebaini kuwa athari za wadudu hao zinetofautiana katika eneo moja la kiikolojia na lingine na kwamba sehemu zenye mvua nyingi mashambulizi hayakuwa mengi kama ilivyo kwenye maeneo yanayopata mvua kidogo ambapo mvua zimechangia Kuwaua," alisema.

Alisema athari za mashambulizi yalikuwa kati ya asilimia 30 hadi 100 kasoro kwenye mikoa ya Njombe,Mbeya na Iringa ambapo yalikuwa asilimia 15.

Dk. alisema mashambulizi yalikuwa makubwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kusini, Mashariki na Rukwa na hivyo kuathiri sana mashamba ya wakulima.

Aliitaja baadhi ya mikoa iliyoathirika na Viwavijeshi Vamizi kuwa ni Iringa, Mbeya, Njombe, Arusha, Kilimanjaro, Simiyu, Geita, Kagera, Tanga, Manyara, Lindi, Mara, Mwanza, Katavi, Rukwa, Morogoro, Singida, Tabora na Songwe.

Rwegasira alisema swala la aina ya mbegu hali kuonyesha tofauti ya mashambulizi kati ya mbegu za asili na chotara maana mashamba yote yaliathiriwa sawasawa bila kujali aina ya mbegu walizotumia hasa baada ya baadhi ya wakulima kusema mbegu za asili hazishambuliwi.

No comments:

Post a Comment

Pages