Katibu Mkuu wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi nchini, Mussa Kabimba, akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya mashine maalum ya kutibu magonjwa ya saratani kwa mionzi. Hafla hiyo imefanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha walemavu wa ngozi nchini, Godson Mwoleli,(wa pili kushoto) akimkabidhi Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Angelina Lutambi (wa pili kulia), mashine maalumu kwa ajili ya matibabu ya saratani kwa njia ya mionzi.
Na Dotto Mwaibale
SERIKALI mkoani Singida, imeahidi kuendelea kupokea changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu wa ngozi na kuzipatia ufumbuzi ili kundi hilo nalo lijione kama jamii nyingine zisizo na ulemavu.
Ahadi hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Angelina Lutambi, wakati akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya mashine maalumu ya kutibu kwa njia ya mionzi kwa walemavu wa ngozi.Mashine hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 8.3 ni msaada kutoka chama cha watu wenye Ulemavu wa ngozi nchini.
Lutambi alisema serikali ya awamu ya tano imeboresha sekta ya afya kitendo kinachopelekea huduma mbalimbali, zipatikane wakati wo wote na bila shida.
Akifafanua zaidi alisema kwa sasa vituo vya afya ikiwemo hospital mbalimbali nchini, vina dawa na vifaa tiba kwa kiwango cha kukidhi mahitaji.
“Huduma za maradhi ya saratani ambazo zilikuwa zikifuatwa Taasisi ya Saratani ya ngozi ya Ocean Road jijini Dar es Salaam sasa zitapatikana mkoani kwetu na hii mashine tunayoikabidhiwa leo,itatumika kutibu watu wenye ulemavu wa ngozi na wale wasio na ulemavu wa ngozi”,amesema Dk.Lutambi.
Amesisitiza kwamba watu wenye ulemavu wa ngozi na wasio na ulemavu,serikali itaendelea kuhakikisha inatoa huduma za afya stahiki kwa Watanzania wote pasipo ubaguzi.
Lutambi ametumi fursa hiyo kukishukuru Chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi Taifa, kwa msaada huo wa mashine hiyo maalumu katika kutibu saratani za aina mbalimbali na kuwa usiwe wa mwisho, waendelee kusaidia mkoa huo ili kuhakikisha wakazi wanakuwa na afya njema na kuweza kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi Taifa,Mussa Kabimba,alisema wameamua kugawa mashine hizo mikoani kwa sababu ya vifo vingi vya watu wenye kansa ya ngozi.
Alisema kazi iliyo mbele yao pamoja na kugawa mashine hizo ni kutoa elimu juu ya maradhi yatokanayo na magonjwa ya kansa ili watu wenye ulemavu wa ngozi waweze kutambua dalili zake mapema na jinsi ya kuyaepuka maradhi hayo.
Katibu wa watu wenye mahitaji maalum mkoani Singida,Ramadhani Maulidi, ametumia nafasi hiyo kuishauri serikali iwaagize wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, manispaa na miji wakati wa kuagiza madawa wahakikishe wanaagiza na mafuta maalumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Wakati huo huo mkazi wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Mariamu Mkumbo,ameziomba mamlaka mbalimbali zisaidie kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa watu wenye changamoto ya maradhi ya ngozi ili waweze kufanya shughuli za ujasiriamali zitakazowasaidia kuwa na uwezo wa kununua mafuta maalumu na dawa zao za kujipaka bila kuwa wategemezi kwa mtu.
No comments:
Post a Comment