Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
amewataka wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao wana nguvu za
kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo wafanye hivyo, ili waweze kujiingizia
kipato badala ya kutegemea ruzuku kutoka Serikalini kupitia TASAF.
Dkt. Mwanjelwa ametoa maagizo hayo alipokuwa
akizungumza na wananchi na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika
vijiji vya Lukindo na Burugo, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera.
Dkt. Mwanjelwa amesema utawekwa
utaratibu maalum ambao kila mwananchi mwenye uwezo wa kufanya kazi ambaye yuko
kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini afanye hivyo na kulipwa ujira kutokana
na kazi atakayoifanya.
“Ni wajibu wa walengwa wote wenye
uwezo wa kufanya kazi ambao wako kwenye mpango huu, wafanye kazi badala ya
kutegemea ruzuku ili nguvu kazi yao isipotee bure,” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Ameongeza kuwa, kufanya kazi kwa
wanufaika hao ni sehemu ya kuwasaidia katika kuboresha maisha yao na kusisitiza
kuwa ruzuku itabaki tu kwa wananchi wasioweza kufanya kazi ambao wengi wao ni
wazee na watoto.
Aidha Naibu Waziri huyo amewataka
wataalam wa halmashauri za wilaya nchini kote kuhakikisha kuwa wanafanya
ufuatiliaji wa karibu kwa wanufaika ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na
tija kubwa.
Dkt. Mwanjelwa anaendelea na ziara
ya kikazi mkoani Kagera kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF na kuhimiza
uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma katika Halmashauri zote za mkoa huo ambapo
tayari ameshatembelea Manispaa ya Bukoba na Halmashauri ya Bukoba Vijijini.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akilakiwa
na wananchi wa kijiji cha Burugo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani
Kagera ambako yuko kwenye ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF na kukutana na Watumishi wa Umma kuhimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
akizungumza na wananchi na Wanufaika wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika
kijiji cha Burugo (hawapo pichani) juu ya utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Baadhi ya Wananchi na Wanufaika wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika katika kijiji cha Lukindo kilichopo
Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (katikati)
akiwa nyumbani kwa mmoja wa walengwa wa TASAF katika kijiji cha Burugo Bi.
Justa Migini (kulia kwa Naibu Waziri) ni Meneja wa Miradi ya
Ajira za Muda TASAF Bw. Paul Kijazi
wakishuhudia nyumba iliyojengwa na mlengwa huyo kwa kutumia ruzuku ya
TASAF.
Mmoja wa Wanufaika wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini wa kijiji cha Burugo, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani
Kagera Bi. Agnes Kemilembe akitoa ushuhuda wa namna alivyotumia ruzuku
kuboresha makazi yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb). Picha ya chini ni
mlengwa huyo akimuonesha naibu waziri shamba lake analoliendeleza kwa kutumia
ruzuku ya TASAF.
No comments:
Post a Comment