Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiangalia baadhi ya Hati
za Ardhi zilizopo Ofisi ya Msajili wa Hati Kanda ya Magharibi wakati wa ziara
yake mkoani Tabora mwishoni mwa wiki. Kulia ni Msajili wa Hati Kanda ya
Magharibi Julian Ngonyani. (PIcha na Wizara ya Ardhi).
Na Munir Shemweta, WANMM TABORA
Idadi kubwa ya Hati za
Ardhi takriban12,000 katika Ofisi ya Msajili wa Hati imemshtua Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipofanya ziara Ofisi
ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi.
Mwishoni mwa wiki Dkt
Mabula akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali
kupitia kodi ya ardhi sambamba na kukagua masijala ya ardhi katika halmashauri
za mkoa wa Tabora alitembelea Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya
Magharibi kujionea utendaji kazi wa kanda inayojumuisha mikoa ya Tabora, Katavi
na Kigoma.
Akiwa Ofisi ya Msajili
wa Hati, Dkt Mabula alielezwa na Msajili wa Hati wa Kanda ya Magharibi Julian
Ngonyani kuwa ofisi yake ina takriban hati 12,000 ambazo ziko tayari kwa ajili
ya kukabidhiwa kwa waombaji lakini wahusika hawajajitokeza kuchukua kwa sababu
ambazo hazijulikani.
Naibu Waziri Dkt Mabula
alishangazwa na idadi kubwa ya Hati hizo na kubainisha kuwa Hati zilizopo Ofisi
ya Msajili wa Hati kama zingechukuliwa basi wahusika wangekuwa na nyaraka
zinazoonesha umiliki halali wa maeneo yao sambamba na hati hizo kuwasaidia
katika shughuli za maendeleo kama vile kukopa pesa katika mabenki mbalimbali.
Alisema, Halmashauri katika
mikoa ya Kanda hiyo ya Magharibi zinapaswa kuwajibika kwa kuhakikisha waombaji
wanapata hati ambapo alizitaka kuandaa utaratibu maalum utakaowezesha Hati kupelekwa
kwenye halmashauri husika na waombaji kuzichukua.
Kwa mujibu wa Dkt
Mabula, utaratibu huo utawawezesha wananchi kuchukua hati zao kwa urahisi bila
ya usumbufu ambapo hivi sasa waombaji hulazimika kuzifuata Ofisi ya Kamishna wa Kanda
jambo alilolieleza kuwa ni usumbufu kwani baadhi ya waombaji hulazimika kutembea umbali mrefu hasa kwa wale
wanaokaa maeneo yaliyo mbali na Ofisi ya Kanda.
‘’Halmashauri inaweza
ikandaa utaratibu wa kupelekewa Hati za Ardhi katika maeneo yao na Ofisi ya
Kamishna wa Kanda na jukumu la halmashauri litakuwa kugharamia pesa ya kujikimu
kwa watumishi wa Kanda watakaopeleka hati na kuzikabidhi kwa waombaji, hiyo
itasaidia kuwapunguzia mzigo wananchi’’ alisema Dkt Mabula.
Katika
Hatua Nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameikabidhi Hati ya Kiwanja No 47 Block
A Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tabora kilichopo eneo la Kanyenye Manispaa ya
Tabora mkoni Tabora baada ya kiwanja hicho kuwa na mgogoro wa muda mrefu Kati
ya ofisi ya CCM na Shirika la Utangazaji (TBC).
Dkt Mabula alimkabidhi
hati hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tabora Mohamed Katete ambapo
makabidhiano hayo yalishuhudiwa na Katibu wa CCM mkoa wa Tabora Solomon Kasaba,
Katibu UWT mkoa Rehema Mohamed, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharbi
Idrissa Kayera na Msajili wa Hati wa Kanda Julian Ngonyani.
Katika Makabidhiano
hayo, Dkt Mabula alisema Chama cha Mapinduzi kina maeneo mengi inayomiliki
lakini siyo yote yenye hati na kubainisha kuwa kukabidhiwa hati hiyo iwe chachu
kwa chama kuhakikisha maeneo yake yote yanakuwa na hati kuepuka migogoro.
Ametoa wito kwa CCM
kuhakikisha maeneo ya Kata yanayomilikiwa na chama hicho yasiyopimwa yanapimwa
na kupatiwa hati na hata yale yasiyo pimwa basi yawe na mipaka na kubainisha
kuwa kwa kufanya hivyo kutaondoa migogoro na kukifanya chama kuwa na miliki
halali ya maeneo yake.
No comments:
Post a Comment