NA SULEIMAN MSUYA, MUHEZA
MRADI
wa Uhifadhi Endelevu na Usimamizi wa Misitu kwa Uhifadhi wa Ndege
Kolokolo Domorefu katika Milima ya Usambara Mashariki umetajwa kukuza
uchumi wa wanavijiji.
Mradi
huo wa uhifadhi Ndege aina ya Kolokolo Domorefu unatekelezwa na Shirika
la Nature Tanzania na wadau mbalimbali chini ya ufadhili wa Critical
Ecosystem Partnership Fund (CEPF).
Wakizungumzia
mradi huo viongozi na wanakijiji wa Kijiji cha Shemomeza, Kata ya
Amani wilayani Muheza mkoani Tanga walisema mradi huo ni mkombozi wa
misitu na maisha ya wananchi.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Shemomeza, Hamisi Baruti, alisema mradi huo umewezesha
wanavijiji kuwapatiwa rasilimali mbalimbali kama mazoa ya viungo,
ng'ombe wa maziwa na nguruwe.
Alisema
pia Nature Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya
Asili Tanzania (TFCG), wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi, watoto wa
shule za msingi na sekondari kutambua umuhimu wa utunzaji misitu na
ndege huyo.
Baruti
alisema wanavijiji wenye misitu inayopakana na Msitu wa Uhifadhi
Mazingira Asili Amani walikubali kukata miti ya Mihesi ambayo sio asili
na kupanda ya asili na mazao ya viungo ili kulinda ndege Kolokolo
Domorefu anaelekea kutoweka.
"Ndege
Kolokolo Domorefu amekuwa fursa nzuri kiuchumu hapa kijijini baada ya
Shirika la Nature Tanzania kuja na mradi wa kumlindaa lakini pia
wanakijiji wamenufaika kiuchumi na mazingira," alisema.
Mtendaji
wa Kijiji hicho Michael Siafu, alisema mradi wa Kolokolo Domorefu
umechochea ujifadhi hali ambayo inasababisha amani kuwa salama
kimazingira.
"Huyu ndege
ni fursa yakipekee hapa kwetu na nchini kwa ujumla Wizara ya Maliasili
na Utalii ikiamua kumtangaza mapato yataongezeka kwa wanakijiji na
nchi," alisema.
Ofisa
Mtendaji wa Kata ya Amani, Hadija Salim alisema ofisi yake imejipanga
kushirikiana na wadau wote ambao wanagusa maisha ya wananchi wakiamini
hivyo ndio mkakati wa kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati.
Aliwataka
wanavijiji wengine kuiga mfano huo wa wenzao kujitolea kutoa maeneo yao
ili kumlinda Kolokolo Domorefu ambaye anatajwa kuadimika.
Mkulima
wa mazoa ya viungo kijijini hapo Amir Said, alisema anawashukuru Nature
Tanzania kumuwezesha mbegu za viungo ili kushirikiana nao kumlinda
ndege Kolokolo Domorefu.
"Nimetoa
eneo langu ili Nature Tanzania wapande miti asili kuwalinda Kolokolo
Domorefu, lakini nimefaidika na mbegu za viungo kama Karafuu, Mdalasini,
Pilipili Manga na Iliki vimeanza kubadilisha maisha yangu," alisema.
No comments:
Post a Comment