Mkurugenzi Msaidizi wa Shirikia la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Emmanuel Lyimo (kushoto), akimkabidhi bango lenye ujumbe wa uhifadhi wa misitu kwa Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Mbomole wilayani Muheza, Rashid Omari, mkoani Tanga.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbomole, wilayani Muheza, mkoani
Tanga, Athuman Singano, akitoa maelezo kuhusu faida za mradi huo
kijijini kwake.
NA SULEIMA MSUYA,
ALIYEKUWA MUHEZA
VIONGOZI na wananchi wa
Kijiji cha Mbomole, Kata ya Mbomole wilayani Muheza mkoani Tanga wameahidi kumlinda
ndege aina ya Kolokolo Domorefu anayepatikana katika Hifadhi ya Mazingira Asili
ya Amani pekee.
Kauli hiyo viongozi na
wanakijiji kuahidi kumlinda ndege huyo ambaye anatajwa kuwa katika kundi la viumbe
hai adimu duninia inakuja baada ya kupatiwa elimu na Shirika la Nature Tanzania
kuhusu umuhimu wa ndege huyo kiuchumi na mazingira.
Mwenyekiti wa Kijiji
cha Mbomole, Athuman Singano, alisema mwaka jana Nature Tanzania iliwaletewa Mradi
wa Uhifadhi Endelevu wa Usimamizi Misitu kwa Uhifadhi wa Ndege Kolokolo
Domorefu katika Milima ya Usambara Mashariki ambapo umekuwa na matokeo chanya.
Singano alisema
wanakijiji wameupokea kwa mikono miwili ambapo wanashiriki kutunza msitu huo wa
aina yake nchini Tanzania huku wakiwekeza katika kilimo msitu kisichoharibu
mazingira.
“Kolokolo Domorefu
ameweza kutukomboa sisi kama wananchi lakini kijiji kimeweza kupata zaidi ya
shilingi 910,000 kwa ajili ya kumalizia ofisi ya kijiji lakini pia tumenufaika
kwa mafunzo kutoka Nature Tanzania wakishirikiana na Shirika la Kuhifadhi
Misitu ya Asili Tanzania (TFCG),”alisema.
Ofisa Mtendaji wa
Kijiji cha Mbomole, Emmanuel Mageta alisema mradi huo wa Nature Tanzania umesababisha
wananchi wote wawe sehemu ya ulinzi wa misitu na mazingira.
“Wapo wananchi
wamewezeshwa kiuchumi katika miradi ya ng’ombe, nguruwe na miche ya mbegu za
mazao ya viungo hivyo matarajio yetu ni siku chache zijazo Mbomole itainuka
kiuchumi,” alisema.
Mnufaika wa mradi huo
Jomo Simon alisema baada ya kuwezeshwa ameanza kuona matarajio yake ya baadae
kimaisha na kuwaomba wananchi wengine kushiriki katika mradi huo.
Simon alisema
anajishughulisha na kilimo cha viungo vya iliki, pilipili manga, karafuu ambapo
mwishoni mwa mwaka huu ataanza kuvuna,
Kwa upande wake kijana
wa miaka 15 Halifa Jumaa alisema mradi huo umemjengea uelewa wa kulinda viumbe
hai akiwemo ndege Kolokolo Domorefu na kuwataka vijana wenzake kumlinda ili
aweze kuchochea uchumi wa kijiji chao.
Meneja Mradi wa Nature
Tanzania, Victor Mkongewa alisema mradi
huo wa kumlinda Kokoloko Domorefu unafadhiliwa na Mfuko wa Kuhifadhi Viumbe
Adimu Duniani (CPEF), umejikita kuhakikisha ndege huyo anaendelea kuwepo
nchini.
Alisema Kolokolo
Domorefu ni ndege adimu ambaye anavutia watalii lakini pia ni ishara tosha kuwa
mazingira yapo salama.
“Kolokolo Domorefu
hawazidi 249 duniani kote hivyo katika kuhakikisha anaendelea kuwepo tumeamua
kuiwashirikisha wananchi wa Mbomole na Shebomeza ambavyo vipo kandokando ya
Hifadhi ya Amani na mwitikio ni mzuri,” alisema.
No comments:
Post a Comment