Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akikabidhi cheti cha ushiriki wa mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamaizi wa Biashara, Daniel Ntigizu, kwa mmoja wa vijana walioshiriki mafunzo hayo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Ofisi ya
Waziri Mkuu imedhamiria kuwawezesha vijana kupitia programu ya mafunzo ya
Ujasiriamali na Usimamaizi wa Biashara kwa lengo la kuwawezesha kukuza na
kurasimisha biashara zao.
Akizungumza wakati wa hafla
fupi ya uzinduzi wa programu ya mafunzo hayo katika Mkoa wa Geita Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa mafunzo hayo ni mahususi kwa
vijana na yatawawezesha vijana kupata elimu juu ya masuala mbalimbali ya
ujasiriamali na biashara ikiwemo urasimishaji wa biashara, kutambua ushindani, upatikanaji
wa mitaji, masuala ya uchambuzi wa
masoko, mikakati na uendeshaji wa biashara.
“Mafunzo haya yanamanufaa
sana kwenu ninyi vijana kwa kuwa yatawawezesha kukua kwa kasi katika biashara zenu
mnazoziendesha na hivyo kuwajengea wigo mpana wa kuendeleza shughuli za
kiuchumi mnazozifanya,” alisema Mhagama
Alifafanua kuwa Ujasirimali
ni moja ya nguzo za sera ya taifa ya uwezeshaji ambayo inalenga kuinua viwango
vya ujuzi na uzoefu wa masuala ya biashara nchini.
Alieleza kuwa, kupitia programu
hiyo vijana 4,000 watanufaika na Mafunzo hayo ambayo yatawajengea uwezo vijana
nchini kuwa na uelewa juu ya masuala ya biashara ikionesha utekelezaji wa azma
ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Magufuli
katika kuwawezesha vijana.
“Ofisi ya Waziri Mkuu
itaendelea kuwajengea uwezo vijana kote nchini kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali katika kutatua changamoto zinazowakabili ili waweze kujiajiri,
kuajiri wenzao kwa ujumla pamoja,” alisisitiza Mhagama
Aliongeza kuwa dhamira ya
Serikali katika kuwawezesha vijana inatekelezwa kwa vitendo kupitia programu
mbalimbali ikiwemo ya ukuzaji ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu,
mmoja wapo ikiwemo ya Mafunzo ya Ujasirimali kwa vijana.
Sambamba na hayo, Mhe.
Mhagama aliwasihi vijana walioshiriki mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kuwa ni
chachu ya mageuzi katika kuboresha biashara zao. Pia aliwataka vijana hao
kueneza ujuzi waliopata kupitia mafunzo hayo kwa vijana wenzao.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa
maagizo kwa viongozi wa Mkoa huo kuhakikisha vijana wanashiriki kwa wingi
katoka mafunzo hayo kwa kuwa yataleta matokeo chanya kwa jamii na yatakuwa ni
chachu kwa vijana katika kujiletea maendeleo sambamba na kuwawezesha kuchangia
pato la Taifa.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya
Nyang’hwale Mhe. Hamim Gwiyama ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo alisema
kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa vijana maana wao ndio nguvu kazi ya taifa,
hivyo kijana akiwa na ujuzi wa mambo mbalimbali ya biashara ni faida kwake
kutambua njia bora za kukuza shughuli zao za uzalishaji mali.
“Katika Mkoa wa Geita vijana
walikuwa na mawazo kuwa dhahabu ndio biashara pekee itakayowapa faida, ila
kupitia mafunzo haya wataweza kutambua kuwa biashara yoyote wakisimamia vizuri
itakuwa na manufaa kwao,” alisema Gwiyama
Naye, Mmoja wa Vijana
walioshiriki katika Mafunzo hayo Bw. Salim Hassan aliweza kutoa shukrani zake
kwa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yameweza kuwatoa katika sehemu moja
na kuwapeleka hatua nyingine.
“Leo tumepata stadi za
msingi katika masuala ya ujasirimali na biashara, tumeweza kuelewa umuhimu wa
kutunza kumbukumbu, usimamizi wa fedha, taratibu za kurasimisha biashara na
jinsi ya kutafuta masoko,” alisema Hassan
AWALI
Programu ya Mafunzo ya
Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara ilizinduliwa rasmi na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama, Jijini Dodoma Julai 29, 2019. Mafunzo hayo
yanasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) katika Mikoa nane (8) ya Tanzania Bara
ikiwemo Dodoma, Ruvuma, Geita, Mwanza, Lindi, Mbeya, Arusha na Tanga. Tayari
vijana kutoka Mkoa wa Dodoma na Ruvuma wamekishwa nufaika na mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment