Baadhi ya Wadau wa Utalii nchini waliokuwa wamehudhuria Kongamano la
Utalii wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe. Constantine Kanyasu wakati akijibu baadhi ya hoja ambazo zilikuwa
zimewasilishwa na wadau hao ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi. ( Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii).
Na Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema
itaendelea kupunguza adha mbalimbali zinazowakabili Wadau wa Utalii
likiwemo suala la polisi wa usalama barabarani kusimamisha magari yenye
watalii mara kwa mara.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine
Kanyasu alipokuwa akizungumza na Wadau wa Utalii nchini katika
kongamano la Utalii lililofanyika mkoani Arusha.
Amesema
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa utalii nchini imejenga vituo vya
ukaguzi wa magari vya utalii ili kupunguza usumbufu kwa watalii
barabarani.
Amesema vituo hivyo vitashughulikia masuala ya msingi likiwemo suala madereva wenye watalii kupimwa kilevi.
Amesema mbali na kilevi, Vituo hivyo vitashughulikia vitendo vyote ya uhalifu watakavyofanyiwa watalii.
Aidha, Mhe.Kanyasu amesema lengo la Serikali ni kupunguza kero kwa watalii ili wafikie milioni mbili mwaka 2019.
Akizungumza
kwenye kongamano hilo, Mhe.Kanyasu amesema licha ya kujengwa vituo
hivyo vya ukaguzi lakini bado kuna kero ambazo zinafanyiwa kazi
lengo likiwa ni kuboresha sekta ya utalii.
Kwa
upande wake, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Jonathan Shana amewataka
wadau wa utalii kufuata sheria lakini akataka kupewa taarifa za polisi
wanaowakwaza.
"Nipigieni simu hata saa nane za usiku kwa askari wanawaomba rushwa nishughulike nao" Alisisitiza Shana.
Naye Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe.Mrisho Gambo amesema lengo la Arusha kuanzisha vituo vya ukaguzi magari ni kupunguza kero.
Amesema uwepo wa vituo hivyo vitafanya mazingira bora kwa watalii na wafanyabiashara.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wasafirishaji Watalii (TATO) Wilbard Chambulo amesema
ujenzi wa vituo hivyo ni hatua muhimu ya kuwahakikishia watalii usalama
wao pindi wakiwa barabani pamoja na mali zao.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Prof.Adolf Mkenda
amesema mkoa wa Arusha ni mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine kwa kujenga
vituo hivyo ili kupunguza kero kwa watalii.
No comments:
Post a Comment