Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, wakati alipowasili kwenye viwanja vya
Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu, katika kilele cha Maonyesho ya 27 ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) 2019.
3647 - Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni
ya NSAGALI ambaye pia ni Mteja wa Benki ya CRDB Mkoani Simiyu, Emmanuel
Silanga alipokuwa akitoa ushuhuda wake wa kuwezeshwa Mkopo uliomuwezesha
kununua Pamba kutoka kwa Wakulima, wakati alipotembelea Banda la Benki
ya CRDB, katika kilele cha Maonyesho ya 27 ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
(Nane N ane) 2019, kwenye Uwanja wa Nyakabindi, Bariadi mkaoni Simiyu.
Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimuelekeza jambo, Mkurugenzi Mtendaji
wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, wakati alipotembelea Banda la Benki
ya CRDB, katika kilele cha Maonyesho
ya 27 ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) 2019, kwenye Uwanja wa
Nyakabindi, Bariadi mkaoni Simiyu.
NA MWANDISHI WETU, SIMIYU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakulima nchini kuchangamkia fursa
zinazotolewa na Benki ya CRDB kupitia akaunti ya “FahariKilimo” ambayo ni
maalum kwa ajili ya wakulima. Akizungumza wakati wa kilele cha maonyesho ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) 2019 nchini iliyofanyika kitaifa mkoani
Simiyu, Waziri Mkuu alisema akaunti hiyo ya “FahariKilimo” ambayo imeambatana
na fursa nyingine za uwezeshaji ikiwamo mikopo kwa wakulima itasaidia kwa kiasi
kikubwa kuboresha mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.
"Serikali
inaridhishwa sana na jitihada kubwa zinazofanywa na Benki hii ya CRDB katika
kuboresha sekta ya kilimo nchini. Ubunifu huu wa huduma na bidhaa mnazozitoa
kwa wakulima nchini unaambatana na dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa
kati wa viwanda ukizingatia malighafi ya viwanda vyetu inapatikana katika sekta
hii mama ya kilimo,” alisema Waziri Mkuu.
Akielezea
mkakati wa Serikali katika urasimishaji wa wakulima ilikuwajengea mazingira
mazuri ya upatikanaji wa mikopo katika taasisi za fedha, Waziri Mkuu alisema
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Wizara ya Ardhi imeandaa mpango mkakati wa
upimaji wa ardhi ya wakulima nchini kote, jambo ambalo pia litasaidia kuongeza
thamani ya ardhi ya wakulima hao.
“Nafahamu
changamoto kubwa inayopelekea riba za mikopo ya kilimo kuwa kubwa ni pamoja na
wakulima kukosa dhamana na mashamba yao kukosa hatimiliki hivyo kuongeza hatari
ya mikopo. Jambo hili tunalifanyia kazi lakini pia niyaombe mabenki yote nchini
kuweka mkakati madhubuti utakaopelekea kupungua kwa riba kwenye mikopo ya
kilimo, riba ikipungua hata wale ambao ni wakopaji wazuri lakini wamekuwa
wakihofia gharama za mkopo nao watakuja kukopa,” alisema Waziri Mkuu.
Abdulmajid
Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, alisema akaunti ya FahariKilimo
ni sehemu ya mkakati mpana wa Benki hiyo kuwahudumia wakulima kwa ukaribu zaidi
kwa kuzingatia mahitaji yao. “Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba nikujulishe kuwa
akaunti hii ya FahariKilimo hufunguliwa bure kabisa na hakuna gharama zozote za
uendeshaji wa akaunti kwa mkulima, tukilenga kumpa mkulima unafuu wa kupokea
malipo yake pindi anapopokea malipo baada ya kuuza mazao,” aliongezea Nsekela.
Nsekela
alisema mpaka sasa wakulima zaidi ya 30,000 tayari wameshajiunga na akaunti ya
FahariKilimo na hivyo kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki ya
CRDB kwa wakulima. “Mkulima anapofungua akaunti ya FahariKilimo tunamuingiza
moja kwa moja kwa mpango wetu maalum wa uwezeshaji ambapo atakuwa akipata
mafunzo mbalimbali juu ya kuboresha kilimo chake kupitia huduma na bidhaa za
Benki yake ya CRDB,” alisema Nsekela.
Nsekela
aliendelea kusema baadhi ya fursa ambazo Benki hiyo imekuwa ikitoa kwa wakulima
ni pamoja na mikopo ya pembejeo, matrekta ya kulimia, mashine za kupandia,
mashine za umwagiliaji, mikopo ya vifaa vya ujenzi pamoja mikopo kwa wawekezaji
katika viwanda vya kilimo.
“Tumekuwa na utaratibu wakushirikiana na wadau
mbalimbali wa kilimo nchini katika kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo za
kisasa zitakazopelekea kuongeza kiwango cha uzalishaji na faida wanayopata.
Kama unavyoona leo hii hapa tupo na wenzetu wa ETC Agro ambao kwa pamoja
tunatoa mikopo ya matrekta kwa wakulima kwa vigezo na masharti nafuu kabisa,”
alisema Nsekela.
Nsekela
alisema ilikupata mkopo huo wa trekta mkulima anatakiwa kuchangia asilimia 35
wakati asilimia 65 itatolewa na Benki ya CRDB ambapo mteja atalipa kwa muda wa
miaka 3. “Katika mkopo huu wa trekta mkulima hahitaji kuwa na dhamana, trekta
litatumika kama dhamana ya mkopo,” alisema Nsekela.
Nsekela
alimwambia Waziri Mkuu kuwa asilimia 40 ya mikopo ya kilimo nchini imetolewa na
Benki ya CRDB, jambo linaloashiria utayari wa Benki hiyo katika kuboresha sekta
ya kilimo nchini. “Kwa mwaka jana pekee Benki ya CRDB kipindi cha mwaka
2018/2019, tumetoa zaidi ya shilingi
bilioni 650 katika kilimo,” alisema Nsekela.
Aliendelea
kusema kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi bilioni 97.3 zilielekezwa kwenye
zao la pamba katika kununua mbegu (bilioni 36) na kulipia pamba (bilioni 61).
Nyingine zilielekezwa katika kilimo cha miwa (bilioni 167.3), Kilimo cha kahawa
(bilioni 36.6), kilimo cha chai (bilioni 60).
“Leo hii
hapa tumeambatana na mteja wetu ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda
cha uchakataji pamba ambacho hivi karibuni tumewapatia mkopo kwa ajili ya
ununuzi wa zao la pamba,” aliongezea Nsekela.
Nsekela
alimalizia kwa kumhakikishia Waziri Mkuu kuwa Benki ya CRDB imedhamiria kwa dhati kuunga mkono sekta ya
kilimo na viwanda ili kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya tano yakufikia
uchumi wa kati unaoshamirishwa na viwanda. “Ahadi yetu kwa Serikali ni Tupo
Tayari,” alihitimisha Nsekela.
No comments:
Post a Comment