Na Talib Ussi, Zanzibar
Katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu katika mazingira
bora Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema itatumia zaidi ya Sh. Bilioni 2
zitatumika kwa ajili ya kununulia madawati ya Skuli za Msingi.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa kujadili hatua iliyofikia juu
ya makusanyo ya fedha za madawati hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya
uhamasishaji ya upatikanaji wa madawati katika Skuli za Serikali, Haroun
Ali Suleiman, ambaye pia Ni Waziri wa Utumishi na Utawala bora Zanzibar alisema kupitia fedha hizo, wanatarajia
kununua jumla ya madawati Kumi na nne elfu na sitini na tano.
Alisema tayari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar, imeshatangaza tenda kwa kampuni mbalimbali ambapo kampuni nne
zimeshachaguliwa za nchini China, na muda mfupi wataalamu watakwenda
kukagua ili kujiridhisha viwango wanavyovihitaji kwa madawati hayo.
“Ifikapo mwishoni mwa Disemba mpaka January mwakani madawati
hayo yatakuwa tayari yameshawasili nchini” alisema Haroun.
Aidha alifahamisha kuwa juhudi
hizo ni miongoni mwa Malengo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk.Ali Mohammed Shein katika kuwasaidia wananchi wake hasa
wanafunzi kusoma katika Mazingira mazuri na salama ili kupata wataalamu zaidi hapa
nchini.
Aidha Mhe Haroun amemshukuru Mhe Rais wa Zanzibar, kwa kuanzisha
kamati hiyo ambayo imeisaidia Wizara ya Elimu juu ya ununuzi wa Madawati
kupitia michango ya wadau mbalimbali nchini ambayo imeweza kufanikiwa kwa kiasi
kikubwa.
Alieleza kuwa madawati hayo ambayo yatakuwa ni awamu ya kwanza yahusisha
Skuli za Msingi ili kusaidia kupunguza
tatizo la madawati katika Skuli mbalimbali Unguja na Pemba.
Pia aliwaomba wananchi wote wa Zanzibar kuendelea
kushirikiana na kushajiishana kutoa michango mbalimbali ili kuwasaidia vijana
wao waweze kusoma katika mazingira mazuri, kwani juhudi hizo zimeonekana kwa
kuweza kuongeza idadi ya ufaulu kwa wanafunzi katika ngazi mbalimbali nchini.
Nae Makamo mwenyekiti wa kamati ya Madawati Riziki Pembe Juma
ameitaka Wizara ya nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na
Idara Maalum za SMZ kuhakikisha wanafanya maandalizi juu ya madarasa
yatakayowekwa madawati hayo kutokana na usalama wa maeneo ya Skuli kwani
zinaonekana baadhi yake hazipo salama kuwekwa madawati hayo.
Kwa upande wao wajumbe wa kamati hiyo walitoa ushauri wao
kuhakikisha ubora wa madawati yatakayonunuliwa yanakuwa na kiwango, kwani upo
uwezekano wa kuchakachuliwa na kusababisha kuingia hasara baadae.
Serikali
zote mbili Tanzania zipo katika mpango maalum wa kuwezesha wanafunzi
kuondokana kukalia sakafu kwa kueneza madawati.
No comments:
Post a Comment