*Basi hilo ni hospitali kamili itakayotoa huduma mkoani Dodoma na mikoa jirani
TAASISI ya Association of African Economy and Development in Japan (AFRECO) imeahidi kuipatia Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma basi ambalo ni hospitali kamili litakalotoa huduma za matibabu kwa Manispaa ya Dodoma, Mikoa na Wilaya zinazoizunguka Mkoa wa Dodoma.
Basi
hilo litakapowasili nchini kutoka Japan linatarajiwa kuwa ni mkombozi
kwa wananchi waishio vijijini na katika maeneo ambayo hayana hospitali
kwani kila litakakokwenda kutoa huduma litakuwa na madaktari waliobobea
katika utaalamu wa tiba mbalimbali, vifaa tiba, maabara pamoja na dawa.
Hayo
yamebainishwa leo (Jumapili, Septemba 1, 2019) na Rais wa AFRECO, Bw.
Tetsuro Yano katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
yaliyofanyika kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan.
Bw.
Yano amesema wameamua kuanza kutoa misaada na huduma zao nchini
Tanzania baada ya kufurahishwa na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha
huduma za afya kwa wananchi.
Ameongeza
kuwa anaamini siku moja Tanzania itakuwa nchi ya mfano kwa Afrika
Mashariki na Afrika yote kwa kutoa huduma bora za tiba kwani itakuwa na
vituo vingi vya Afya na hospitali zenye uwezo wa kutibu magonjwa kama
vile ya moyo na figo. Hata hivyo tayari wagonjwa toka nchi jirani
wameanza kuja kutibiwa nchini.
Kwa upande wake,
Waziri Mkuu amesema mbali na kutoa basi ambalo litakuwa linatoa huduma
za matibabu, pia taasisi hiyo ya AFRECO itasaidia katika kupandisha
hadhi hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa Shule
kamili ya tiba.
Amesema
hospitali hiyo ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma itapatiwa
vifaa mbalimbali vya tiba ambavyo vitaifanya hospitali hiyo kuwa ni
shule bobezi kwa utoaji wa tiba mbalimbali nchini Tanzania na Barani
Afrika.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema kuwa wamekubaliana na AFRECO kuanzisha kitivo
maalum cha Uhandisi wa Vifaa Tiba ambacho kitafundisha uhandisi wa vifaa
tiba ili nchi yetu iwe na watalaamu wa kukarabati vifaa tiba pindi
vinapoharibika badala kuvipeleka nje ya nchi au kuagiza wahandisi na
watalaamu kutoka nje ya nchi kuja kuvitengeneza.
“Hivi
sasa yanafanyika makubaliano ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza
vifaa tiba na kwa kuanzia wataanza kutengeneza maji ya drip ambayo
huongezwa kwa wagonjwa kwa maeelekezo ya madaktari na baadae watengeneza
dawa mbalimbali.”
Naye,Naibu
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mipango, Utawala na Fedha,
Profesa Donald Mpanduji amesema wametia saini hati ya makubaliano kati
ya AFRECO na Chuo Kikuu cha Dodoma ambayo yanalenga kuboresha hospitali
ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
Awali,
Dkt. Omary Ubuguyu kutoka Wizara ya Afya amesema maboresho yaliyofanywa
na Serikali ya Awamu ya Tano katika huduma za tiba yameiwezesha
Tanzania kupunguza wagonjwa wanaopelekwa nchi za nje kwa matibabu kutoka
800 hadi 42 ambalo ni punguzo la asilimia inayotajwa kuwa 200.
Amesema
hatua hiyo imeongeza nafasi kwa watalaamu wetu wa tiba kujifunza zaidi
pamoja na kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri kwenda nje ya nchi
kutafuta tiba na pia imeipunguzia Serikali gharama ya fedha za kigeni
ambazo zingetumika kuwatibu wagonjwa nje ya nchi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa , Rais wa The Association of African Economy and Development in Japan (AFRECO), Bw. Tetsuro Yano (kushoto) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mipango, Utawala na Fedha, Profess Donald Mpanduji (kulia) wakishikana mikono ikiwa ni ishara ya makubaliano yanayolenga kuboresha hospitali ya Chuo Kuu cha Dodoma ya Benjamin Mkapa kati ya Chuo hicho na AFRECO baada ya mazungumzo yao kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan, Septemba 1, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais wa The Association of African Economy and Development in Japan (AFRECO), Tetsuro Yano, kabla ya mazungumzo yao leo kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais wa The Association of African Economy and Development in Japan (AFRECO), Tetsuro Yano, kabla ya mazungumzo yao leo kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment