Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu
Kijaji (Mb).
Na Peter Haule na Saidina
Msangi, WFM, Dodoma
Serikali
imetoa wito kwa wadau wote wa kilimo nchini
kuwasiliana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo –TADB ili waweze kupata maelekezo
sahihi ya uandaaji wa miradi itakayokidhi vigezo vya kupatiwa mikopo na benki
hiyo.
Wito
huo umetolewa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji,
alipokuwa akijibu swali la Msingi la
Mbunge wa Mbeya Vijijini ,
Mhe. Oran Njeza,
aliyetaka kujua mkakati wa Benki ya
Kilimo kuwafikia wakulima wadogo wa Wilaya ya Mbeya.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa, Benki ya TADB
imefikisha huduma zake mkoani Mbeya na kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kutoka
Sh. milioni 799.9 mwezi Desemba 2017 hadi Sh. bilioni 2.54 kufikia Aprili, 2019.
Alisema kuwa mikopo imetolewa kwa miradi 7 ya kilimo na
kuwanufaisha wakulima 509 wa Nyanda za Juu Kusini katika wilaya za Mbozi, Momba
na Mbalali.
“Benki ya TADB imefanikiwa kufungua Ofisi ya Kanda ya
Nyanda za Juu Kusini Mkoani Mbeya, lengo likiwa kuhakikisha Benki hiyo
inasogeza huduma zake karibu zaidi na wateja ambao ni wakulima wote wa Nyanda
za Juu Kusini, ikiwa ni pamoja na wakulima wadogo wa Wilaya ya Mbeya Vijijini”,
alieleza Dkt. Kijaji.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa ili kuhakikisha kuwa Benki ya TADB inakuwa na fedha za
kutosha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima, Serikali imeipatia benki hiyo
kiasi cha Sh. bilioni 103, kupitia mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya
Maendeleo ya Afrika- AfDB.
Aidha kwa sasa Benki hiyo inaendelea na mchakato wa
kukamilisha masharti ya kupatiwa awamu ya pili ya mkopo wa Sh. Bilioni 103
kutoka Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika.
Benki ya TADB tangu ilipoanza rasmi shughuli zake
mwaka 2015, TADB imefanikiwa kujiendesha na kukuza mtaji wake hadi kufikia Sh.
Bilioni 67.5 zilizo rekodiwa mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2019 kutoka
Sh. Bilioni 60 mwezi Novemba, 2014.
No comments:
Post a Comment