*Miss Tanzania 2019 aahidi kutumia kiswahili mashindano ya Miss World
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amemtaka Miss Tanzania 2019, Sylivia Bebwa (19) ahakikishe anakuwa balozi mzuri wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali na aishi kwa kuzingatia utamaduni wa Mtanzania.
“Miss
Tanzania lazima awe mbunifu na uelewa mpana katika masuala mbalimbali
zikiwemo jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo ya
wananchi kama kuhamasisha elimu hususan kwa watoto wa kike ili waweze
kutimiza ndoto zao.”
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Septemba 11, 2019) wakati
alipokutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.
Harrison Mwakyembe, waandaaji wa mashindano ya Miss Tanzania, Miss
Tanzania na mshindi wa pili na watatu wa shindano hilo, ofini kwa Waziri
Mkuu Mlimwa jijini Dodoma.
Amesema
Miss Tanzania anatakiwa kutumia fursa hiyo kutangaza vivutio mbalimbali
vya utalii vilivyopo nchini, shughuli zinazofanywa na Serikali katika
kukuza uchumi pamoja na kuhamasisha wananchi washiriki katika kufanya
kazi kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema Miss Tanzania pamoja na washiriki wengine wa
mashindano hayo wanatakiwa waishi kwa kuzingatia utamaduni wa Mtanzania
ikiwemo kuwa na nidhamu katika jamii ili waweze kuwashawishi wengine
kushiriki.
Waziri
Mkuu amempongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.
Mwakyembe kwa namna anavyoratibu shughuli mbalimbali katika wizara hiyo.
“Hata katika sekta ya michezo viwango vimeanza kuonekana.”
Waziri
Mkuu amesema Serikali inaunga mkono masuala ya michezo na inapenda
kuona viwango vinapanda, hatua ambayo itawawezesha wahusika kufanya
vizuri katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki.
Kwa upande wake,
Waziri Dkt. Mwakyembe amemshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuonana na
ujumbe huo hususani Miss Tanzania ambaye anajiandaa kwenda kushiriki
katika mashindano ya Miss World yanayotarajiwa kufanyika London,
Uingereza Desemba 14 mwaka huu.
Waziri
huyo amesema miaka ya nyuma Serikali haikuridhishwa na namna mashindano
hayo yalivyokuwa yakiendeshwa lakini kwa sasa hali ni tofauti na
yamekuwa na viwango vya kimataifa. Mashindano hayo kwa sasa yanasimamiwa
na aliyekuwa Miss Tanzania 2008, Basilla Mwanukuzi kupitia kampuni ya
The Look.
Naye,Mwandaaji
wa Mashindano hayo, Basilla Mwanukuzi ametumia fursa hiyo kuishukuru
Serikali kwa ushirikiano inaoutoa kwao na pia ameiomba izidi kuwaunga
mkono kwa kuwa watatumia mashindano hayo katika kulitangaza Taifa.
Awali,
Miss Tanzania 2019, Sylivia ameishukuru Serikali kwa fursa aliyopewa ya
kukutana na Waziri Mkuu na alisema kuwa atajitahidi katika kuhakikisha
anatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo kuiwakilisha Tanzania kwenye
mashindano ya Miss World na kwamba anakwenda kutumia lugha ya kiswahili.
“Nimefurahi
kwa heshima hii niliyopewa na Serikali ya kukutana na Mheshimiwa Waziri
Mkuu, naahidi kwamba niyatekeleza maagizo yote aliyoyatoa ikiwa ni
pamoja na kuishi kwa kuzingatia maadili ili wazazi wengine waweze
kuwaruhusu watoto wao washiriki katika mashindano haya kwani urembo ni
heshima.”
No comments:
Post a Comment