NA SULEIMAN MSUYA
KATIKA kuhakikisha kuwa
rasilimali misitu nchini inakuwa endelevu Mradi wa Mkaa Endelevu Tanzania
(TTCS), umetengeneza igizo la ‘Misitu Yetu Maisha Yetu’ ili kulinda rasilimali
hiyo muhimu kwa maisha ya viumbe hai.
Akizungumzia igizo
hilo, Ofisa Uhusiano wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG),
Bettie Luwuge alisema wameamua kuja na mfumo wa igizo ili elimu ya uhifadhi
misitu iweze kusambaa zaidi.
Luwuge alisema igizo
hilo ambalo limetengenezwa katika mazingira ya vijiji vinavyojihusisha na
Usimamizi wa Misitu ya Shirikishi ya Vijiji (USM), limejikita katika utoaji wa
elimu zaidi.
“Sisi TFCG ambao ndio
wawezeshaji wa mradi wa TTCS tumeamua kuja na igizo lenye ujumbe wa USM
tukiamini rasilimali misitu itakuwa salama kwani wananchi wengi watanufaika
zaidi,” alisema.
Alisema igizo hilo
limeshirikisha waigiza wakubwa na wadogo ambapo matumaini yao ni kuona ujumbe
unafika kwa haraka kwa jamii.
Ofisa Uhusiano huyo alisema
matarajio yao ni kuona wananchi wanashiriki katika USM ili kuweza kunusuru
misitu ambayo ina mchango mkubwa katika maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake Ofisa
Uraghibishaji wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita), Elida Fundi alisema igizo hilo
ambalo limejikita katika kuongelea hali halisi ya uharibifu wa misitu nchini litakuwa
linarushwa katika vituo vya televisheni na redio ili kufikia wananchi wengi
zaidi.
“Tumeamua kutumia njia
ya igizo ili kuanisha visababishi vikuu vya uharibifu wa misitu kwenye ardhi za
vijiji na namna mpango shirikishi wa misitu unavyochangia kupunguza upotevu wa
misitu,” alisema.
Fundi aliwataka
wananchi kufutialia vipindi vya televisheni kuanzia kesho kwenye televisheni za
ITV, EATV na nyinginezo ili kupata elimu hiyo muhimu ya USM.
Alisema iwapo jamii
kubwa itapata uelewa wa USM ni dhahiri misitu itakuwa salama na malalamiko ya
manadiliko ya tabia nchi ambayo yanalalamikiwa kila mara yatakuwa
yamedhibitiwa.
No comments:
Post a Comment