HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 10, 2019

Blueink yatoa somo kwa vyombo vya habari

Mkurungezi Mkuu wa Kampuni ya Matangazo na Mawasiliano ya Blueink, Amin Swai, akizungumza na wahariri na waandishi wa habari waandamizi wa habari jijini Dar es Salaam.
 

NA SULEIMAN MSUYA

VYOMBO vya habari vya magazeti, redio na televisheni vimeshauriwa kuwekeza katika mfumo wa kidijitali ili kuweza kuongeza wasomaji, wasikilizaji, watazamaji na watangazaji wa matangazo.

Ushauri huo umetolewa na Mkurungezi Mkuu wa Kampuni ya Matangazo na Mawasiliano ya Blueink Amin Swai, wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari waandamizi wa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam.

Swai alisema uingiaji wa mfumo wa kidijitali nchini umekuwa changamoto kubwa kwa vyombo vya habari hasa magazeti kupata matangazo hivyo njia yakuweza kushawishi watoa matangazo ni kuhakikisha wanawekeza katika mfumo huo.

Alisema takwimu zinaonesha jamii inatumia mitandao ya kijamii kupata taarifa na habari za kila siku hivyo vyombo vya habari vinapaswa kubadilika na kuendana na hali ilivyo duniani kwa sasa.

“Naomba wamiliki wa vyombo vya habari hasa magazeti, redio na televisheni kubadilika kwa kuwekeza katika mfumo wa kidijitali ambao ndio umeshika sekta ya mawasiliano duniani inaweza kuwa njia sahihi ya kuongeza wasomaji na watangazaji,” alisema.

Alisema Blueink imejipanga kutumia nafasi yake kuhakikisha vyombo vya habari nchini vinapata faida kupitia habari na matangazo hivyo kuviomba viendeleze ushirikiano.
Mkurugenzi huyo alisema thamani ya vyombo vya habari ni kubwa hivyo ni vema kuwepo mipango ambayo itafanya wanaohusika na vyombo hivyo wasione kuwa wanapoteza muda.

Alisema pamoja na vyombo hivyo kuwekeza katika mfumo wa kidijitali idara zinazohusiana na mauzo na matangazo zinapaswa kuwa na ubunifu ili kuweza kufikia wateja wengi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma, Ibraham Kyaruzi alivishauri vyombo vya habari kupanua masoko na kuongeza nakala za magazeti ili kushawishi watangazaji kwenye vyombo vyao. 

“Ni kweli vyomvo vya habari hasa magazeti vinapitia wakati mgumu ila sisi kama watu wa masoko na mawasiliano tunawashauri mtafakari namna ya kuongeza nakala ili muweze kufikia kundi kubwa,” alisema.

Kyaruzi alisema asilimia kubwa ya wananchi wanatumia mitandao ya kijamii hivyo ili kuweza kushindana nayo ni vema kuwepo na mikakati miziru ambayo itawezesha kushawishi watangazaji kukubali kutangaza na chombo chako.

No comments:

Post a Comment

Pages