Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Mganga Biswalo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI wa Mashtaka Nchini (DPP), Biswalo Mganga, amestushwa
baada ya kubaini kuwapo kwa baadhi ya mawakili wanaokwenda gerezani na
kuchukua fedha kwa washtakiwa wanaokabiliwa na kesi za uhujumu uchumi
kwa kusema kuwa wanakwenda kuwalipia katika ofisi yake jambo ambalo
amesema si kweli.
Mganga amesema mawakili hao
wanatafuta ugomvi na Ofisin yake na wasije wakamlaumu kwani ni miongoni
mwa watu wanaotumika kukwamisha mchakato wa msamaha uliyotolewa na Rais
John Magufuli hivi karibuni kwa washtakiwa hao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, DPP Mganga alisema tayari ameshaanza kufanya uchunguzi ili kuwabaini mawakili wanaofanya kazi hiyo ya utapeli.
"Leo
(jana) nimepata taarifa juu ya uwepo wa baadhi ya mawakili wanaochukua
fedha kutoka kwa washtakiwa na kusema wanazileta kwa DPP, naomba
niwakanye na niwaonye wanaofanya hivyo maana wanatafuta ugomvi, tusije
kulaumiana kwani nimeshaanza kufanya uchunguzi, niwasihi wafanye
shughuli zao za uwakili na kuheshimu ofisi ya DPP," alisema Mganga.
Alisema utaratibu wa mshtakiwa kukiri upo pale pale na kusisitiza kuwa watu hao wanapaswa kufuata taratibu za kisheria za mahakama.
Aidha
Mganga alisema taratibu za kulipa fedha zipo mahakamani na sio wakili
ama mtu yoyote kutoka na kwenda gerezani au kumfuata ndugu wa washtakiwa
na kuwaambia awapatie fedha.
“Huo
utaratibu haupo katika mchakato kama huu, naona kuna wajanja wajanja
wanajitokeza wanaotaka kufanya uhalifu katika zoezi hili wajiandae
tutapambana nao wala hatutawavumilia,” alisema DPP Mganga
Hata hivyo, Mganga alisema Serikali imeamua
kufungua akaunti maalumu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa lengo la
kuwawezesha washtakiwa wanaoandika barua za kukiri makosa hayo ya
uhujumu uchumi na kuamriwa kurudisha fedha kulipia kwenye akaunti hiyo.
"Hii
sio akaunti ya mahakama ni akaunti maalumu imefunguliwa BoT kwa amri ya
serikali viongozi wakuu wa mahakama watajulishwa, hivyo hakuna fedha
itakayolipwa katika akaunti ya mahakama, kwa DPP ama Mamlaka ya Mapato
Nchini (TRA),” alisema Mganga.
Mganga
alisema ambaye atalipa sehemu nyingine wasilaumiane kwani lazima fedha
hizo ziende zinapotakiwa na kusisitiza kuwa si mawakili wa Serikali,
watumishi wa ofisi ya DPP au mtu yeyote atakayefanya vitendo vya rushwa
watakayemvumilia.
“Ninasema
hivi sisi hatutamvumilia mla rushwa kama wakili wa kujitegemea ni
mzuri sana mahakamani unakula rushwa hatutakuvumilia ama wakili wa
serikali ni mzuri sana mahakamani unawasilisha hoja unakula rushwa
hatutakuvumilia,” alisema Mganga
Hata
hivyo Mganga alisema watu wote wanaofanya uhalifu katika kipindi hiki
cha washtakiwa walioambiwa kuomba msamaha kwa kuwaibia fedha zao kupitia
ndugu au washtakiwa wenyewe waache.
Septemba
30, mwaka huu, Rais Magufuli aliongeza muda mwingine wa siku saba kwa
watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi na kuwataka wote waliogoma kufuata
masharti hayo, vinginevyo hatatoa muda zaidi baada ya siku hizo
alizoongeza kumalizika.
Rais Magufuli
alitoa onyo hilo Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kupokea
taarifa ya DPP Mganga kuhusu agizo alilotoa la kutaka watuhumiwa wa
uhujumu uchumi kukiri makosa, kuomba radhi na kukubali kurudisha fedha
ili waachiwe huru.
Septemba 22 mwaka huu Ikulu
jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali
aliowateua hivi karibuni wakiwemo mabalozi, makatibu wakuu na makatibu
tawala wa mikoa, Rais Magufuli alimshauri DPP kuangalia uwezekano wa
kuwaachia huru washtakiwa baada ya kukiri makosa na kukubali kurudisha
fedha wanazodaiwa kukwapua.
DPP alisema ofisi
yake imepokea barua 467 za watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi
waliokuwa tayari kukiri na kurudisha fedha walizowaibia watanzania.
Alisema
barua hizo ziliendelea kufika ofisini kwake hadi Jumamosi (Septemba
28,2019) na Jumapili (Septemba 29,2019) kwa sababu zingine zilichelewa
kufika kutoka mikoani.
Alisema kati ya
washtakiwa hao kundi la kwanza lipo tayari kurudisha Sh. Bilioni 7.8
muda wowote kuanzia Septemba 30, mwaka huu, huku washtakiwa wengine
ambao kesi zao zipo kwenye mfumo wa dola za Marekani nao wapo tayari
kurudisha dola zaidi ya Milioni mbili ambazo ni sawa na Sh. Billioni 5.7
za kitanzania.
Alisema kundi lingine la pili
lipo tayari kulipa kwa awamu ambao wataweza kulipa Sh. Bilioni 94.2 na
kuongeza kundi hilo lipo tayari kurudisha fedha hizo kwa awamu kadri
watakavyokubaliana nao kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Aidha
alisema kundi la tatu ni la watuhumiwa wengine wa kesi hizo ambao wapo
tayari kulipa moja kwa moja bila kulipa kwa awamu ambapo fedha
wanazoweza kulipa ni kiasi cha Sh. Bilioni 13.6.
Alisema
jumla ya fedha zote za washitakiwa 467 wenye kesi hizo za uhujumu
uchumi ambao wapo tayari kurudisha ni Sh. Bilioni 107.8 ambazo
watazirudisha serikalini kwa utaratibu watakaokubaliana nao.
No comments:
Post a Comment