HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 06, 2019

RAIS DKT. MAKUFULI AFUNGUA BARABARA YA TUNDUMA –SUMBAWANGA KM 223.21 KATIKA ENEO LA LAELA MKOANI RUKWA

Rais John Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli (wa tatu kulia aliyeshika utepe), viongozi wa Mkoa wa Rukwa, Mawaziri, viongozi wa Dini pamoja na Chama, akikata utepe kuashiria ufunguzi wa barabara ya Tunduma-Sumbawanga kilometa 223.21 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami katika sherehe zilizofanyika leo Laela mkoani Rukwa. (Picha na Ikulu).
Sehemu ya Barabara ya Tunduma–Sumbawanga km
223.21 iliyofunguliwa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika eneo la Laela mkoani Rukwa. 



NA FARAJA EZRA
 
RAIS John Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa Taasisi za kiserikali kuhama kwenye nyumba za kupanga na kuhamia katika nyumba za serikali ili kupunguza gharama za ulipaji kodi.

Akitoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa barabara ya lami kutoka Tuduma hadi Sumbawanga mkoani Rukwa yenye kilomita 223.1 ambayo iligharimu zaidi ya shilingi bil. 406.2 pekee.

Rais John Magufuli alisema ni muda muafaka kwa Taasisi zote za serikali nchini kuhamia kwenye nyumba za serikali kama ilivyo elekezwa.
 
Alisema kumekuwa na gharama isiyokuwa ya lazima kwa taasisi hizo kuendelea kuishi kwenye nyumba za kupanga wakati serikali ina nyumba za kutosha.

Licha ya hayo, Rais John Magufuli amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, kutekeleza agizo la Waziri Kangi Lugola la kuwatoa askari Polisi 9 walioshindwa kutekelezwa majukumu yao.

Alisema askari hao wameshindwa kusimamia haki za wananchi wa mkoa huo baada ya wananchi kuwaletea malalamiko ya kuibiwa mifugo yao.

Aidha malalamiko hayo yamedumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi.

Raisi John Magufuli amemtaka RPC huyo kuacha kupuuza maagizo ya Waziri na kutekelezwa kama yalivyoamriwa.

" Ila watu mnadharau hivi agizo linatolewa haitekelezwi, hivi nikifanya uamuzi wangu utaendelea kuwa katika nafasi hiyo? nasa nakupa onyo katekeleze agizo hilo" alisema Rais John Magufuli.
 
Katika uamuzi mwingine Rais Magufuli ameitaka Jeshi la Polisi kuwasaka waliochoma mradi wa maji mkoani humo ili kuwapeleka Mahakamani.

Aidha Rais Magufuli ametoa siku saba kwa jeshi hilo kuhakikisha watuhumiwa hao wanakamatwa na kupelekwa Mahakamani ili kujibu Mashtaka yanayowakabili.

Awali Rais Magufuli alisema serikali imetoa zaidi ya shilingi bil.7.1 katika ujenzi wa mradi huo ili kuwawezesha wananchi wa mkoa huo kupata huduma ya maji safi na salama.
 
"Lakini cha kushangaza fedha hizo zimetumika bila mradi huo kukamilika na mhandisi aliyekabidhiwa jukumu hilo ameonekana kuchelewesha ujenzi huo, alisema na kuongeza kuwa.
 
"Sasa natoa amri kwa jeshi la Polisi kumtafuta mhandisi huyo wa kampuni ya Fally Enterprises ya mkoani humo, kumkamata na sitakubali mchezo huo uendelee katika serikali ninayoiongoza," alisema Rais John Magufuli.
 
Ifike mahali kila mtu awe mlinzi wa mwenzake ili kuzipa mianya ya uhujumu uchumi katika nchi yetu na taifa kwa ujumla.
 
Alisema haiingiii akilini wananchi walionichagua wateseke kwa ajili mtu mmoja asiyejielewa ni lazima wafaidi matunda ya uchaguzi wao, hivyo ni lazima niwahudumie bure.
 
Rais John Magufuli alipokuwa akizindua mradi huo alieleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa asilimia kubwa na kutaka Wafanya biashara kufanya bidii katika shughuli za uzalishaji mali.
 
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 223.1 inaunganisha miji mitatu ikiwamo Tunduma, Laela na Sumbawanga na kunganisha mikoa ya Mbeya na Rukwa kupitia mji mdogo wa Tunduma.
 
Rais Magufuli alisema mradi huo wa barabara umedhaminiwa na serikali ya Marekani kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili kuboshesha shughuli za usafirishaji nchini.
 
Pia aliwataka watumiaji wa barabara kutunza miundombinu hiyo ili kukuza shughuli za biashara kwa maendeleo ya taifa.
 
Pia amewataka wananchi pamoja na madereva kuendesha vyombo vya moto bila kuharibu taa za barabarani na kutunza vifaa vyote vilivyowekwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu.
 
Naye Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Isaac Kamwelwe, alisema uwepo wa barabara hiyo utasababisha kukuza shughuli za biashara katika mkoa huo lakini pia kwa mikoa ya jirani.
 
Waziri Kamwelwe alieleza barabara hiyo itarahisisha shughuli za usafirishaji wa bidhaa kutoka ndani ya nchi hadi nchi za nje ikiwamo Kongo, Malawi na Zambia.
 
Pia itachochea maendeleo ya nchi kutokana na kurahisishia shughuli za kitalii nchini .
 
Alisema serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya barabara kwani ndiyo sekta muhimu inayochangia ukuaji wa maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Pages