*Asema ikithibitika ni
kweli, lazima warudishe fedha hizo
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Bw. Adili
Elinipenda achunguze watumishi 48 waliojihusisha na upotevu wa fedha kwa njia
za udanganyifu.
Ametoa agizo
hilo leo jioni (Jumapili, Oktoba 6, 2019), wakati akizungumza na madiwani na
watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwenye mkutano uliofanyika kwenye
ukumbi wa Halmshauri hiyo.
Waziri Mkuu
ametoa maeneo saba ambayo ametaka yafanyiwe uchunguzi wa kina ili kubaini
upotevu huo. Eneo la kwanza ni upotevu wa makusanyo ya ndani kupitia mawakala
wa ukusanyaji mapato (POS) ambapo mawakala wanaokusanya fedha wanashirikiana na
watumishi wa Halmashauri na kuzitumia bila kuziingiza benki.
Kuna kundi la
watumishi 10 wakiongozwa na mtu wa TEHAMA, wameshirikiana kupata password na
fedha zikishakusanywa wanazitoa na kuzitumia bila kuzipelekea benki. Wamesahau
kwamba malipo yalipoingizwa mara ya kwanza, data ilirekodiwa kwenye mfumo wa
malipo na sisi tunaona ni kiasi gani kimekusanywa.”
Watumishi hao
ni Salum Omari (Mtaalamu wa TEHAMA); Adam Mzengi (Mhasibu kahamishiwa Gairo);
Rafaeli Nasari; Caroline Makundi (kahamishiwa Singida Manispaa), Edson S. Ally
(Afisa Biashara); Martin Kimisho (Mhasibu Msaidizi); Prosper Banzi (Afisa
Biashara); Hassan Ponda (Mhasibu kituo cha afya Ndago); Hafidh Ngayunda (Kaimu
Mweka Hazina wa Wilaya) na Muhidin Mohammed (Mweka Hazina wa Wilaya) ambaye
tayari amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma hizo.
Kutokana na
upotevu huo, Waziri Mkuu ameagiza Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya akae pembeni
hadi uchunguzi wa TAKUKURU utakapokamilika.
Akibainisha
mchezo mwingine uliochezwa na watumishi wa Halmashauri hiyo, Waziri Mkuu
amesema kuna watumishi 38 ambao walilipwa kiasi cha sh milioni 46 ambazo
zilikuwa sehemu ya sh. milioni 400 za kujenga vituo vya afya vya Ndago na
Kinampanda wilayani humo.
“Hapa nina
vocha zote za malipo walipeana fedha watu hawa akiwemo Mkurugenzi wao. Lakini
ni kazi gani ambayo kundi lote hili lilikuwa likiisimamia na kustahili kupata
malipo hayo? Kutoka makao makuu ya wilaya hadi Ndago au Kinampanda kuna umbali
gani?” alihoji Waziri Mkuu.
“Kamanda wa
TAKUKURU fanya uchunguzi, fuatilia wote waliohusika sababu majina tunayo, kama
hawastahili kulipwa ni lazima warudishe fedha yetu. Hii ni sehemu ya sh.
milioni 90 ambazo hazijulikani ziliko na zilikuja kujenga kituo cha afya. Fedha
hizi zimekuja na maelekezo rasmi, ni kwa nini zilibadilishwa matumizi,”
alihoji.
Waziri Mkuu
alisema kuna fedha ya walimu sh. milioni 29 ambayo ilitumwa na TAMISEMI ili
kulipa likizo zao lakini Mkurugenzi alitumia kulipia usafirishaji wa makontena
ya vifaa vya tiba kutoka Sweden hadi Singida wakati mkataba wa malipo unasema
Halmashauri ilipaswa kulipia kutoka bandari ya Tanga hadi Singida.
“Hii fedha ya
walimu ya likizo nataka irudishwe mara moja. Pia kuna shilingi milioni 6.86
ambazo mmedai ni malipo ya kukomboa mizigo bandarini wakati vifaa hivyo
vilipata msamaha wa kodi. Tena kuna sh. milioni 34 ambazo zililetwa kurekebisha
Ikama za walimu lakini hadi leo hazijalipwa. “Kamanda wa TAKUKURU nataka
uniambie nafasi ya Afisa Elimu ikoje kwenye suala hili,” alisema.
Pia alisema
kuna fedha kujenga machinjio ya kisasa ambayo ililetwa lakini machinjio
hayajakamilika hadi sasa. “Tumeleta sh. milioni 100 za machinjio lakini Afisa
Mifugo anasema wametumi sh. milioni 20 tu, nataka sh. milioni 80 zimeenda
wapi.”
Waziri Mkuu alisema
kuna sh. 18,090,000 za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kutoka vituo vya afya 13
ambazo zimetumika kusafirisha hayo makontena nayo pia irudishwe. “Hivi
mnachangisha watu sh. 30,000 kwa ajili ya kupata dawa wakienda kutibiwa lakini
leo hawana dawa kwa sababu mmezitumia ndivyo sivyo na wao hawana dawa kwenye
vituo hivyo kwa sababu hamjazirejesha.”
“Kamanda wa
TAKUKURU fanya uchunguzi kwenye fedha ya mikopo ya akinamama, vijana na wenye
ulemavu ambayo ni asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri. Fedha hii haijatoka
tangu mwaka 2017/2018 na 2018/2019.
No comments:
Post a Comment