HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 12, 2019

Serikali yatumia Bil.13.7/- kukarabati Chuo Kikuu Mzumbe

 Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Lugano Kusiluka, akizungumza na wanahabari waliomtembelea ofisini kwake.


Na Irene Mark, Morogoro

KIASI cha Sh. Bilioni 13.7 kimetumika kufanya ukarabati na maboresho kwenye Chuo Kikuu Mzumbe jambo ambalo halijafanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 1970.

Mwaka 1954 kilianzishwa na Serikali ya Mkoloni kikiwa Kituo  kwa ajili ya kuwaandaa viongozi wa Vijiji enzi hizo kabla ya kuwa Chuo Kikuu cha Uongozi (IDM) Mzumbe chini ya Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza na Wanahabari waliotembelea shule alizosoma, kufundisha na vyuo vya kimkakati alivyoanzisha hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Lugano Kusiluka, alisema ukarabati mkubwa umefanyika chuoni hapo.

Alisema ukarabati huo umeongeza ufanisi, ikama ya watumishi na kutarajia idadi kubwa zaidi ya wanafunzi hasa baada ya kuwepo kwa ongezeko la mabweni kwenye kampasi zake tatu za Mbeya, Dar es Salaam na kampasi kuu ya Morogoro.

"Haijapata kutokea tangu kuanzishwa kwa Chuo hiki Serikali kuwekeza kwa ukubwa wa namna hii... tunamshukuru sana Rais John Magufuli na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Profesa Joyce Ndalichako, wameweka alama bora kwenye chuo hiki kilichoanzishwa kimkakati na baba wa taifa enzi hizo.

"Wakati wa vuguvugu la ukombozi watanganyika wachache sana walipata elimu hasa waliotoka kwenye familia za machifu, sasa baada ya Uhuru Mwalimu Nyerere akaona upo ulazima sasa wa kuwa na viongozi wasomi ndio mwaka 1970 akakifanya Mzumbe kuwa chuo cha viongozi watakaosimamamia sekta mbalimbali," alisema Profesa Kusiluka.

Alisema mwaka 2001 kwa shetia namba 15 Bunge lilipitisha Chuo cha Uongozi Mzumbe, kuwa Chuo Kikuu rasmi na kuifanya nchi hii kuwa na vyuo vikuu vitatu baada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu Huria (OUT).

Kwa mujibu wa Makamu huyo mkuu wa chuo, kinachofanywa na Serikali ya awamu ya tano kwenye sekta ya elimu, ni mambo ambayo baba wa taifa alitaka sana yafanyike hivyo njia sahihi ya kumuenzi ni kuboresha zaidi elimu.

Baadhi ya maboresho yaliyofanyika chuoni hapo ni Ujenzi wa mabweni yatakayobeba wanafunzi 1,024 kwa wakati mmoja, nyumba 22 za watumishi, majengo na mabweni kwenye kampasi ya Mbeya, ujenzi wa chuo eneo la Tegeta kampasi ya Dar es Salaam.

Alisema wamefanikiwa pia kulipa deni la Sh. Bilioni 2.9 huku akisisitiza kwamba uwekezaji huo mkubwa unatokana na fedha za walipakodi wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Pages