HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 09, 2019

Shirika la Posta Tanzania latakiwa kuisaidia Serikali

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dk. Jimmy Yonazi, akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania (hawapo pichani) wakati wa kilele za maadhimisho ya miaka 150 ya shirika hilo duniani.


Na Janeth Jovin

WIZARA ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imesema kuwa Shirika la Posta Tanzania linawajibu wa kuisaidia Serikali katika kuharakisha maendeleo kwa kurahisisha mawasiliano kupitia huduma za barua, nyaraka, vipeto na vifurushi ndani na nje ya nchi.

Aidha Wizara imesema shirika hilo limekuwa likirahisisha  upatikanaji wa huduma za kifedha za uwakala hasa maeneo ambayo hayafikiwi kirahisi na Kampuni na taasisi zinazotoa huduma za kibiashara.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia mawasiliano Dk. Jimmy Yonazi wakati wa siku ya kilele cha maadhimisho ya miaka 145 ya Umoja wa Posta duniani.

Dk. Yonazi amesema shirika hilo la Posta Tanzania linalojukumu la msingi la kutoa huduma za posta kwa watu wote hivyo ni muhimu likaendelea kuboresha mikakati yao ili liweze kuwafikia watanzania kote nchini.

"Kama mnavyofahamu tupo katika awamu ya tano ya Serikali inayowataka watu kufanya kazi, shirika hili ambalo linamilikiwa na serikali kwa asilimia 100 lina wajibu wa kufuata kauli mbiu hiyo kwa vitendo, kwa kuhakikisha huduma zinazotolewa ni bora na za uhakika kwa wateja wote, " amesema.

Amesema shirika hilo haliwezi kukwepa kuwa moja ya watumiaji wakuu wa mifumo ya kompyuta na mitandao kwani ndiko dunia ilipo kwa sasa.

Naye Kaimu Postamasta Mkuu wa shirika hilo,  Mwanaisha Said amesema wamejizatiti na kuboresha baadhi ya huduma zao ambazo nyingi kwa sasa zinafanyika kidigitali ili kufanikisha jamii kidigitali kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Aidha amesema kwa mwaka huu wamepata mwitikio mkubwa kutoka Tanzania bara na visiwani katika kushiriki shindano ambapo jumla ya wanafunzi 1881 walijitokeza ikilinganishwa na 850 walioshiriki mwaka jana.

"Washindi katika shindano hili wa kwanza ni Joan Erasto kutoka shule ya Sekondari ya Binza iliyopo Simiyu, wa pili ni Grace Kahimba kutoka Shule ya msingi ya St Ann's ya Morogoro na mshindi wa tatu ni Hasnein Rizwan wa Shule ya Almuntazir Boys Seminari ya jiji Dar es Salaam, " amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Shirika hilo, Dk. Harun Kondo amesema shirika hilo limesimama na kuzalisha faida kwa sasa kutokana na mshikamano uliyopo kati ya bodi na wafanyakazi.

No comments:

Post a Comment

Pages