HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 08, 2019

Takukuru Temeke yataja maeneo yanaongoza kwa vitendo vya rushwa

Na Janeth Jovin

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)  Mkoa wa Temeke imesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai mwaka huu, taasisi zilizoongozwa kulalamikiwa kuwa na vitendo vya rushwa katika mkoa huo  ni Manispaa ya Temeke,  Mahakama, polisi, ofisi za Serikali za mitaa pamoja na mabaraza ya ardhi yaliyopo katika manispaa hiyo.

Aidha taasisi hiyo imesema katika kipindi hicho jumla ya taarifa 58 zinazohusiana na vitendo vya rushwa walizipokea na wanefanikiwa kuokoa kiasi cha zaidi ya Sh. Milioni 37.9.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Naibu Mkuu wa Takukuru Temeke, Ramadhani Ndwatah (pichani) amesema katika taarifa hizo walizozipokea majalada mapya ya uchunguzi yaliyofunguliwa na kufikia hatua ya uchunguzi wa kina ni saba.

Aidha amesema kiasi cha Milioni 37.9 walichokiokoa kimetoka katika miradi ya maji iliyopo Somangila Kigamboni ambapo walibaini mkandarasi wa mradi huo alilipwa fedha mara mbili hivyo kumtaka areje fedha  alizolipwa awamu ya pili.

"Pia fedha hizo zimetokana na fedha za mfuko wa jimbo la Temeke ambazo zilitolewa lakini hazikutumika, eneo la mishahara hewa ambapo tulikokoa kiasi cha Milioni 6.7, pia tulikoa fedha za chanjo ya surua ambazo Nazi hazikutumika, " amesema.

Amesema katika kipindi hicho wamefanikiwa pia kufungua kesi nne na kuongeza kuwa bado wanaendelea na majukumu yao ya kuelimisha umma kwa lengo la kuwahamaisha kushiriki kwa vitendo katika mapambano dhidi ya rushwa.

"Uelimishaji ulifanywa kwa kuendesha semina 17 kwa makundi mbalimbali na mikutano ya hadhara 38 kwa wananchi na kuandika makala mbili inayohusiana na vitendo vya rushwa, " amesema.

Hata hivyo amesema katika kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali ya Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba mwaka huu, wamejipanga kuelimisha wananchi na wadau wa uchaguzi wakiwemo wasimamizi, wanahabari, viongozi wa dini pamoja na vyama vya siasa.

"Elimu itakayotolewa inalenga kuwaeleza jinsi ya kujiepusha na vitendo vya rushwa na pia kuwataka washiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutupa taarifa kila wanapoona vitendo vya rushwa kuelekea katika uchaguzi huo, " amesema.

Aidha amesema pia wataendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali hasa yanayolalamikiwa na kuwaeleza wananchi kuhusu umuhimu wa kuzuia vitendo vya rushwa katika chaguzi za kisiasa.

"Pia tunatoa wito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika kufichua vitendo vya rushwa kwa kupiga simu ya bure 113 au kufika ofisini kwani kwa kufanya hivyo titaitokomeza kabisa rushwa na kuinua zaidi uchumi wetu, " amesema.

No comments:

Post a Comment

Pages