HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 08, 2019

Vyuo vyatakiwa kufundisha vijana watakaoshindana katika soko la ajira

Na Janeth Jovin

KATIBU  Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Saimon Msanjila amesema kuwa vijana wengi  waliopo nchini wanashindwa kushindana katika soko la ajira kutokana na kutoandiliwa vizuri.

Amesema kutokana na changamoto hiyo  wameamua Chuo cha Madini kilichopo mkoani Dodoma kilelewe na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa lengo la kuhakikisha nchi inapata wataalamu wa kutosha katika sekta ya madini watakaoshindana kwenye soko la ajira.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kusaini mkataba na UDSM wa kukilea chuo hicho cha madini, Msanjila alisema wameamua kufanya hivyo kwa lengo la kuongeza ufanisi wa taalamu na mafunzo kwa vitendo katika chuo hicho.

 Alisema Wizara hiyo ya madini inaliona suala hilo la kulelewa na UDSM ni muhimu kwa sababu ya ubora uliyopo katika chuo hicho  na kukua kwa kasi kwa sekta ya madini nchini.

"Suala hili la Chuo cha madini kulelewa sio la kwanza tulishaanza huko nyuma ila lilisuasua kutokana na kushindwa kuweka maslahi ya watanzania mbele, leo tumeamua kulelewa ili watanzania waweze kunufaika na kupata elimu bora," alisema na kuongeza

Historia ya UDSM inajulikana vyuo vingi vimelelewa katika chuo hichi na sasa hivi vinatoa elimu bora, sina wasiwasi na matarajio ya Wizara ya Madini kwamba si muda mrefu tutakuwa bora na kujitangaza kimataifa na kuanza kupokea wanafunzi wengi kutoka nje kuja kusoma katika chuo chetu, " alisema

Aidha aliisema ni matumaini yake UDSM watakwenda kuangalia hali ya sasa kwa maana walimu,  mitaala na miundombinu iliyopo katika chuo hicho kwa lengo la kukisaidia ili vijana wapate elimu bora.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo alisema UDSM inasifa ya ubora wa taaluma na hakijawahi kuteteleka hivyo uamuzi wa Chuo cha Madini wa kulelewa na chuo hicho ni sahihi.

"Tunaahidi kama Wizara tutahakikisha Chuo cha Madini kinapata malezi bora kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwani kinauzoefu wa kutosha katika kuvilea vyuo,  kwa lengo la kuwapa ujuzi wa kutosha wanafunzi ili wawe na tija katika soko la madini, " alisema.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye alisema sekta ya madini itegemee kupata wataalamu waliobora na kuongeza kuwa wataongeza udahili ili kukidhi mahitaji ya soko.

Prof. Anangisye alisema chuo hicho cha madini kwa kulelewa na UDSM, kitapata fursa ya kukua na kuingia katika wigo mpana zaidi wa kitaaluma na kuongeza kuwa watawapa uwezo walimu wa chuo wa kufanya tafiti.

"Sisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tumegusa Nyanja nyingi za kitaaluma ikiwemo taaluma ya madini. Idara yetu ya jiolojia imetoa wataalam wanaoheshimika duniani na imekuwa na mchango mkubwa sana kitaifa.

 “Kwetu jukumu hili litatupeleka karibu zaidi na watanzania ambalo ndio lengo letu. Hivi sasa chuo kikuu cha Dar es Salaam kimeendelea kupanua wigo wake na kina matawi mikoani lengo likiwa ni kuwa karibu na watanzania,” alisema.

Kwa upande wake Kamishna wa Madini David Mulabwa alisema anakishukuru UDSM kwa kulikubali  jambo hilo kwani ni hatua muhimu ambayo itaongeza ufanisi wa taaluma kimafunzo na vitendo katika chuo cha madini.

 Alisema hatua hiyo ni kukipa chuo cha madini fursa zaidi ya kutoa mafunzo kwa vitendo katika chuo cha madini.

No comments:

Post a Comment

Pages