Wanariadha wa Tanzania, kutoka kulia Agustino Sulle, Stephano Huche na
Alphonce Simbu, wakimsikiliza Kocha wao, Andrew Panga, mara baada ya
kuwasili leo Doha, Qatar kwenye mashindano ya Dunia.
Na Mwandishi Wetu
NYOTA watatu wa Riadha Tanzania wakiongozwa na Alphonce Simbu
wamewasili salama jijini Doha, Qatar tayari kwa kinyang’anyiro cha mashindano
ya Dunia ‘IAAF World Championships’.
Msafara huo wa Tanzania ukiwa na Nahodha Simbu kutoka Jeshi
la Wananchi Tanzania (JWTZ), Agustino Sulle wa klabu ya Talent na Stephano
Huche wa African Ambassador Athletics Club (AAAC), chini ya Kocha Andrew Panga,
uliwasili majira ya saa nane usiku wa kuamkia leo Oktoba 3 na kupokelewa na
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday.
Gidabuday, alisema vijana wako salama na baada ya kuwasili
walipumzika na jana asubuhi walikwenda kupasha misuli na kujionea hali ya hewa. “Vijana wote wako na hali nzuri, hawana wasiwasi kwani tayari
Failuna alishawafanyia utafiti na wanajua namna ya kukabiliana na hali ya joto
iliyoko huku,” alisema Gidabuday.
Naye Nahodha Simbu alisema kwa ufupi; “Tunashukuru Mungu
tumefika salama, tumeishaona hali ilivyo na tupo tayari kwa kazi iliyotuleta
hapa. Watanzania watuombe,”.
Kwa upande wake, Kocha Panga ambaye pia ni Kocha wa Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT), alisema wachezaji wako salama na wana ari ya kufanya vema,
tayari wameishapata vitendea kazi vyote na wapo tayari kulipigania Taifa.
Tanzania, ilianza vibaya mashindano hayo usiku wa kuamkia
Septemba 28 katika mbio za Marathon Wanawake, pale Failuna Matanga aliposhindwa
kumaliza mbio hizo na kuishia Kilomita 21.
Sasa kete za mwisho zimebaki
kwa Wanariadha hao watatu, ambao watachuana katika Marathon Kilomita 42.195
hapo Oktoba 5, huku Simbu akiwa anatetea medali yake ya Shaba aliyoitwaa katika
mashindano yaliyopita huko London, Uingereza.
No comments:
Post a Comment