HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 03, 2019

BEI YA MBOLEA YASHUKA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari Jijini Dar es salaam katika Ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo  tarehe 3 Octoba 2019 kwa ajili ya kutangaza bei elekezi ya mbolea ya kukuzia (UREA) kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).

 
 
NA TATU MOHAMED 

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imetangaza kushuka kwa bei ya mbolea ya kukuzia (Urea) kutoka Sh. 57,482 hadi kufikia Sh. 53,997 kwa mfuko wa Kilogramu 50 sawa na asilimia sita, katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2019/2020 kuanzia Oktoba Mosi, mwaka.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya bei elekezi ya mbolea ya Urea katika msimu wa kilimo 2019/2020.

Amesema mbolea hizo za kukuzia zimepungua bei kwa asilimia kati ya sita hadi 17 kulingana na umbali na kuongeza kuwa mbolea zinazopatikana nchini kwa sasa bei yake ipo chini ukilinganisha na bei ya dunia.

“Sote tunafahamu kuwa bei ya Urea zinaonekana zimepanda sana ukilinganisha na maeneo mengine lakini kwakuwa tumetumia utaratibu wa ununuzi wa pamoja bei imeshuka kwa kiwango kidogo,” amesema na kuongeza.

“Wizara ilianzisha mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) na kufuta kodi mbalimbali na tozo mbalimbali ambazo zilikuwa kero kwa wakulima wetu  na kuanzisha utaratibu wa kusimamia usafirishaji wa mbolea kutoka maeneo mbalimbali hasa bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoani na kuweka bei elekezi,” amesema.

Waziri Hasunga ameongeza kuwa serikali imeweka utaratibu wa kutoa bei elekezi kwa mbolea aina mbili pekee kati ya mbolea tano ambazo  ni mbolea ya kupandia na mbolea ya kukuzia(Urea).

Amesema mfuko wa kilogram 50 kwa Mkoa wa Dar es Salaam utakuwa unauzwa kwa sh. 45,280 kutoka sh. 48,500 kwa mwaka jana huku kukiwa na punguzo la sh.3,220.

Hasunga amefafanua kuwa Mkoa wa Arusha itauzwa kwa sh. 53,722 kutoka sh 57,236 kwa mwaka jana kukiwa na punguzo la sh. 3,509 huku Geita itauzwa kwa sh. 56,683 wakati kwa mwaka jana iliuzwa sh. 60,124 punguzo likiwa sh.3,440.

Amesema Mkoa wa Iringa bei elekezi ilikuwa sh. 56,443 mwaka jana  ambapo sasa itauzwa kwa sh. 53,934 sawa na punguzo la sh. 3,509, Manyara bei elekezi ilikuwa 58,339 sasa itakuwa sh. 54,830.

Ametaja pia bei ya rejareja kwa mikoa ya Kanda ya Mashariki, Kati, Kusini na Kaskazini zitakuwa kati ya sh. 47,100 hadi sh 55, 800 huku Mikoa ya Kanda ya Magahribi, Nyanda za juu Kusini na Ziwa bei elekezi itakuwa kati ya sh . 52, 400 hadi sh . 59,700.

Amefafanua kuwa bei elekezi hutofautiana na umbali wa eneo moja hadi lingine huku anayefanya tofauti anakiuka sheria huku akibainisha kuwachukulia sharia na kumnyang’anya leseni.

“Kwa mujibu wa sheria ….mbolea zote zinatakiwa kuuzwa kwa bei zilizopangwa na serikali hasa hizi ambazo zinazoingizwa kwa mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja,”alisema.

Waziri Hasunga amesema mfumo wa ununuzi wa pamoja unamanufaa ukilinganisha na makampuni ya kibiashara hivyo vyama vya ushirika vinapaswa kujiunga kwa pamoja na kuagiza kwa pamoja.

Aidha ametoa onyo kwa makampuni yatakayokiuka taratibu kwa kuuza mbolea nje ya nchi bila kufuata utaratibu wa kupewa kibali kuuza nje ya nchi kuwachukulia hatua na kunyang’anya leseni.

“Kuna baadhi ya kampuni yamekuwa yakijiuhusisha na uuzaji wa mbolea zisizo kidhi viwango(fake), itakayopatikana tutawachukulia wahujumu uchumi na hatua kali tutawachukulia dhidi yao,” amesema.

No comments:

Post a Comment

Pages