Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akimhoji
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Godfrey Sanga, kutokana na
matumizi mabaya ya fedha za Umma, Oktoba 5.2019. wakati alipozungumza na Watumishi
wa Halmashauri pamoja na Madiwani, katika ukumbi wa Halmashauri ya Mkalama, mkoani Singida. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu).
*Agoma kuweka jiwe la msingi la hospitali ya wilaya hiyo
*Agoma kuweka jiwe la msingi la hospitali ya wilaya hiyo
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Bw. Adili
Elinipenda amchunguze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama, Bw. Godfrey Sanga
kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.
Baadhi ya
tuhuma alizonazo ni kujilipa posho ya safari Machi mwaka huu bila kusafiri,
kuwasainisha watumishi wa chini yake vocha na kisha kuwapa ‘asante kidogo’ kwa
madai fedha hizo zinaenda mkoani, kujilipa stahiki kabla ya wakati na kuagiza
gari liende gereji kwa matengenezo bila nyaraka zozote.
Ametoa agizo
hilo leo jioni (Jumamosi, Oktoba 5, 2019), wakati akizungumza na madiwani na
watumishi wa Halmashauri hiyo kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa
Halmshauri hiyo.
“Kuna
watumishi wanne uliwaambia wasaini vocha ya sh. 1,320,000. Hii ni kwa safari
iliyopangwa kati ya tarehe 15 na 24 Septemba, mwaka huu; ukawapa asante ya sh.
30,000 ukidai kuwa zinatakiwa mkoani. RAS ni kweli hela hiyo ililetwa mkoani?” Alihoji
Waziri Mkuu na kujibiwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. Anjelina Lutambi kwamba
hakutoa hayo maagizo.
Alipoulizwa Mweka
Hazina wa Wilaya hiyo, Bw. Peniel Mbula kwamba fedha alilipwa nani, mweka
hazina huyo alijibu kwamba alikuwa Dodoma kikazi. Mhasibu aliyekaimu nafasi
yake, Bi. Lulu Hamadi aliwataja watumishi hao kuwa ni Stella Mawa, Godfrey Mnubi,
Richard Laizer na Method Kafuku.
Waziri Mkuu aliwasimamisha
watumishi hao na kuwauliza walilipwa hiyo posho ili waende wapi lakini walikosa
majibu. Ndipo akawaeleza kwamba walimkabidhi Mkurugenzi na wakalipwa asante ya sh.
30,000.
Alipoulizwa
kuhusu malipo ya sh. 1,090,000 ambayo yalilipwa Septemba 9, mwaka huu yalikuwa
ya nini, Mkurugenzi huyo alijibu kuwa ni ya stahiki zake za kila mwezi ambapo
kati ya hizo, sh. 600,000/- ni za malipo ya nyumba; sh. 230,000 ni za umeme na sh. 260,000 ni za simu. Lakini
hakuweza kujibu ni kwa nini amejilipa kabla mwezi haujaisha.
Kuhusu gari
la elimu lenye namba za usajili STK 913 lililopelekwa gereji kupakwa rangi kwa
gharama ya sh. milioni saba, Waziri Mkuu alitaka aoneshe dokezo lililotumika
kupitisha idhini hiyo na malipo hayo lakini akajibiwa kwamba hakuna utaratibu
wa kuandika dokezo pindi magari ya Halmashauri yanapoenda kufanyiwa matengenezo
bali wanapeana taarifa kwa mdomo tu.
“Kamanda wa
TAKUKURU leta maafisa kutoka mkoani waje wafanye ukaguzi wa kila jambo ambalo
limeainishwa. Hatuwezi kuacha Halmashauri iendeshwe kienyeji bila kufuata
taratibu. Mkalama inaonekana chafu kumbe tatizo ni mtu mmoja, mnasaini vocha
halafu mnamsingizia RAS,” alisema.
“Ajenda ya
kikao changu nanyi watumishi wenzangu, nilitaka tuambiane kwamba ni lazima
tutunze mali na fedha za Serikali. Waheshimiwa Madiwani ni lazima msimamie Halmashauri
yenu na mhoji kila senti imetumika vipi. Kama ni jengo nendeni mkakague, kama
ni kisima nendeni mkaangalie,” alisisitiza.
“Pia niwasihi
Waheshimiwa Madiwani wenzangu, msikubali kutumika kupitisha matmizi ya fedha
ambayo si sahihi,” aliongeza.
Watumishi wa
Halmashauri hii mfanye kazi, muache ubabaishaji sababu Serikali hii iko makini
sana. Msiishi kwa mazoea, kwa sababu wakati siyo wenyewe na tena muache
kutengezeza syndicates,” aliwaonya.
Pia amemuonya
Afisa Manunuzi wa wilaya hiyo, Bw. Dickson Mataramba aache kutumika na kufanya
kazi kwa mazoea kwa kupandisha bei ya sh. elfu 2000 hadi 3,000 kwenye vifaa
wanavyoagiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amekataa kuweka jiwe la
msingi la Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya kwa sababu lilikataliwa na
Kiongozi wa mbio za Mwenge na uchunguzi wake bado haujakamilika.
“Jiwe la
msingi mlilonipangia kuweka leo kwenye hospitali ya wilaya siweki hadi TAKUKURU
wakamilishe kazi ya uchunguzi kuhusu mikataba iliyotumika. Mkikamilisha
uchunguzi mniite, nitakuja kulizindua likiwa limekamilika,” amesema.
No comments:
Post a Comment