HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 11, 2019

Wizara ya Elimu yakarabati shule aliyosoma Nyerere

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma shule ya Msingi Mwisenge aliyosoma Mwalimu Nyerere wakiwa mbele ya bweni alilolala baba wa taifa kati ya mwaka 1934 hadi mwaka 1936.
 Fundi mwashi akiwa kwenye ukarabati wa baadhi ya majengo ya shule ya Msingi Mwisenge alikosoma baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere
Sehemu aliyopenda kukaa Mwalimu Nyerere akiwa mwanafunzi wa shule ya Mwisenge mkoani Mara.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sylvia Lupembe, akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea shule alizosoma na kufundisha hayati baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Mwisenge ni moja ya shule za zilizotembelewa.
Sehemu ya Uzio wa Shule ya Msingi Mwisenge uliojengwa wakati wa ukarabati wa shule hiyo ambayo Hayati Mwalimu Nyerere alisoma kati ya mwaka 1934 hadi mwaka 1936.
 
 
Na Irene Mark, Musoma

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetumia Sh. Milioni 772.6 kukarabati Shule ya Msingi Mwisenge, Wilaya ya Musoma mkoani Mara, alikosoma Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Ukarabati huo umehusisha uzio kuzunguka shule hiyo, madarasa 29, bwalo la chakula, bweni jipya la wanafunzi 80, nyumba tatu za walimu moja kati ya hizo inabeba familia mbili na zahanati ya shule.

Akizungumza na wanahabari waliotembelea shule hiyo aliyosoma baba wa taifa, Mwalimu Mkuu wa Mwisenge B, Jones Lumbe, alisema ukarabati huo ulianza Aprili mwaka huu na kubainisha kwamba utamalizika mwanzoni mwa Novemba.

Alisema kabla ya ukarabati huo, hali ya majengo ya shule ilikuwa mbaya huku mengine yakoshindwa kutumika kutokana na ubovu wake.

"Mwanzoni mwaka huu Rais John Magufuli, alitembelea shule hii akaona uchakavu wa shule yetu alitembelea kila mahali alisikitika sana akaagiza ufanyike ukarabati.

"Siku chache baada ya ziara ya Rais Magufuli, alikuja Waziri wa Elimi, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akaangalia hali ilivyo akafanya tathimini na kuahidi kuanza ukarabati mapema.

"...Tulichelewa kidogo kuanza ukarabati kwa sababu ya watu wa mambo ya kale hasa kwenye bweni na darasa alilosoma Mwalimu Nyerere. Hata hivyo ulifika mwisho ukarabati ukaanza.

"Ukitembelea utaona kuna umeme, sakafu nzuri kwa kweli tumekuwa na vitu vipya," alisema Mwalimu Lumbe.

Alisema Mwalimu Nyerere alianza masomo katika shule ya Mwisenge, Aprili 20 mwaka 1934 na kuondoka shuleni hapo Oktoba Mosi mwaka 1936 baada ya kufanya na kufaulu mtihani wa darasa la nne akiwa darasa la tatu.

"Shule ilianzishwa mwaka 1924 kwaajili ya watoto wa machifu na wakati anaingia hapa Kambarage alikuwa mtoto mwenye akili sana alipofaulu mtihani alipelekwa shule ya elimu ya juu huko Tabora," alisema Mwalimu Lumbe.

Aliitaja namba ya usajili wa Mwalimu Nyerere kuwa ni 308 huku akisisitiza kwamba mwanafunzi huyo alikuwa akiishi shuleni hapo.

No comments:

Post a Comment

Pages