HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 09, 2019

Kampeni 'Linda Ardhi ya Mwanamke' kuzinduliwa Novemba 21

Mchambuzi wa Masuala ya Ardhi kutoka Shirika la Kimataifa la Landesa, Khadija Mrisho akitoa mada katika mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu kampeni ya 'Linda Ardhi ya  Mwanamke' mafunzo hayo yalifanyika mjini Morogoro.


NA SULEIMAN MSUYA, MOROGORO

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anatarajiwa kuzindua Kampeni ya 'Linda Ardhi ya Mwanamke' Novemba 21 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Hayo yalisemwa na Mchambuzi wa masuala ya Ardhi kutoka Shirika la Kimataifa linalochochea na kuangazia ulinzi wa haki za ardhi za kijinsia kwa waliopo mijini na vijijini – Landesa, Khadija Mrisho wakati wa mafunzo kwa wanahabari kutoka mikoa mbalimbali Tanzania yanayofanyika mkoani Morogoro

Alisema, Tanzania ni nchi ya kwanza kuanza kutekeleza kampeni hiyo kutokana na kuwepo kwa utashi wa kisiasa na ushirikiano wa Taasisi za kiraia na Serikali kwa ujumla zinazoangalia ni namna gani haki za mwanamke zinalindwa.

Alisema Landesa inashirikiana na taasisi zingine za kirai kama Tamwa, Tala, TNRF na nyingine kuhakikisha mwanamke ana kuwa na haki ya kumiliki ardhi kama sheria inavyotaka.

Alisema wamemchagua Waziri Ummy kuzindua kampeni hiyo wakiamini kuwa ni mtu sahihi katika eneo hilo hivyo wanatarajia kupata ushirikiano kwa wananchi kampeni ikianza.

Alisema kampeni hiyo ambayo inazinduli nchini kwa mara ya kwanza itakuwa ya miaka 12 ila itatekelezwa kwa miaka mitatu mitatu.

"Kampeni hii ya ,'Linda Ardhi ya Mwanamke ' ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa kundi hilo ambalo takwimu zinaonesha ni asilimia 24 ndio wanamiliki ardhi huku asilimia 80 wakishiriki shughuli za kilimo,"alisema.

Mrisho alisema matarajio ya taasisi zote amabazo zinashiriki kampeni hiyo, ni kuona inakuwa endelevu kwa kufikia kundi kubwa la wanawake wasiomiliki ardhi..

Aidha alisema, Kampeni hiyo ilizinduliwa kimataifa kwenye mkutano wa benki ya Dunia nchini Marekani mwezi March 2019 ambapo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi kitaifa Novemba 21 mwaka huu jijini Dar es salaam ambapo Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kwa majaribio.

Mwanasheria wa Shirika la Landesa, Godfrey Massay amewaasa wanawake kuzingatia na kuzitumia sheria zilizopo ili kuweza kupata haki zao na kuachana na mtazamo wa kusubiri haki kutoka kwa mtu.

Alisema sheria namba 4 -5 ya mwaka 1999 ya ardhi za vijiji inatambua umiliki wa ardhi wa kati ya mwanamke mwenyewe na mwanaume kwa pamoja hivyo ni jukumu la wanawake wote kuitumia sheria hiyo.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zina sheria nzuri za masuala ya usimamizi wa ardhi na kutambua haki za mwanamke.

"Sheria hizi zimepewa jina la mapinduzi ya mfumo dume zina vifungu vizuri ambavyo vikitekelezwa vinavyoweza kuondoa changamoto ya haki za mwanamke katika umiliki ardhi," alisema.

Eda Sanga ambaye ni Mmoja wa Wakurugenzi wa Bodi ya Ladesa  alisema mafunzo hayo kwa waandishi ni msingi mzuri wa kufanikisha mapambano hayo.

Sanga alisema kampeni hiyo itajikita kutoa elimu zaidi hivyo kupitia vyombo vya habari ni imani yake wanawake wengi watafikiwa.

No comments:

Post a Comment

Pages