HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 09, 2019

VPL YAZIDI KUWA KAA LA MOTO KWA MAKOCHA, MAYANJA NAE 'OUT' KMC

Jackson Mayanja
Aliyekuwa kocha wa KMC, Jackson Mayanja.
Na Mwandishi Wetu
 
UONGOZI wa klabu ya KMC ya Kindondoni jijini Dar es Salaam, umefuata nyayo za waliokuwa wawakilishi wenzao wa Tanzania katika michuano ya klabu barani Afrika, baada ya leo kutangaza kumvunjia mkataba kocha wake Jackson Mayanja.

KMC, inayomilikiwa na Halmashauari ya Manispaa ya Kinondoni, ilishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC), pamoja na Azam FC, ambayo ilishaachana na kocha wake, Etienne Ndayiragije na nafasi yake kuchukuliwa na Aristica Cioaba wa Romania.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya KMC, ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta, klabu yake imeamua kuachana na Mayanja, raia wa Uganda kwa kile alichokiita ‘maendeleo yasiyoridhisha kwa timu yao tangu kuanza kwa msimu huu.’

Sitta amebainisha kuwa, maamuzi ya kusitisha kandarasi ya mwaka mmoja ya Mayanja iliyosainiwa Juni 26 mwaka huu, hivyo kuitumikia timu kwa siku 136 (sawa na miezi mitatu na nusu), yalifikiwa baada ya makubaliano ya pande zote mbili (uongozi wa timu na kocha).


“Uamuzi wa kusitisha kandarasi ya Mayanja ni makubaliano baina ya pande zote mbili, na hii ni kutokana na muendelezo wa matokeo yasiyoridhisha ya timu yetu tangu kuanza kwa msimu huu wa 2019/20.


“Tunamshukuru Kocha Jackson Mayanja kwa mchango wake mkubwa alioutoa akiwa na timu. KMC FC inamtakia Mayanja kila la kheri katika majukumu yake mapya nje ya klabu yetu,” imesema taarifa ya Sitta juu ya uamuzi wa kuachana na Mayanja.

Mayanja alichukua nafasi ya Ndayiragije, aliyetimkia Azam FC, kisha kukakimu nafasi ya kuinoa timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars,’ huko akichukua mikoba ya Mnigeria Emmanuel Amunike, kabla ya kupewa jukumu rasmi la kuinoa timu hiyo.

Baada ya Azam FC kuachana na Ndayiragije, waliokuwa wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL) na baadaye CAF CC, Yanga, waliachana na Mwinyi Zahera na nafasi yake kujazwa kwa muda na Charles Mkwasa, kabla ya KMC nayo jana kufuata nyayo.

Mayanja anaondoka KMC akiwa ameiongoza timu hiyo kucheza mechi mbili za CAF CC na kutupwa nje, huku akiiongoza kucheza mechi nane za Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), ambako juzi ilichapwa na Kagera Sugar, kichapo cha nne, wakishinda mbili na sare mbili msimu huu.

Ukiondoa Zahera na Ndayiragije, Mayanja pia anafuata nyayo za Malale Hamsini wa Ndanda FC, Athuman Bilali ‘Bilo,’ Alliance FC na Fredy Felix ‘Minziro’ wa Singida United.

Kwa sasa KMC sasa wapo nafasi ya 16 katika VPL, wakiwa na pointi nane, nne juu ya Singida United inayoburuza mkia wa ligi hiyo ya timu 20.

No comments:

Post a Comment

Pages